Ninatembea usingizini. Nina tatizo? (Sleep Walking)

Wakati tumelala usiku, ninashtuka na kumuona rafiki yangu amesimama mbele ya kitanda chake akiduwaa. Ninamwita kwa nguvu lakini haitikii. Mara nyingine hutoka kitandani na kutembeatembea wakati macho yamefumbwa. Muda mwingine huniangalia kabisa machoni lakini bila kunitambua. Nikijaribu kumuongelesha, hunyamaza kimya au kusema mambo yasiyoeleweka. Huweza hata kufungua kabati na kubadilisha nguo, au kufungua friji na kula kisha kurudi kulala. Nikimweleza kesho yake kile alichokifanya, hukataa na kusema nilikuwa ninaota tu.

Kutembea usingizini mara nyingi hutokea wakati mtu amelala usingizi mzito, masaa kadhaa baada ya kulala. Huweza kutokea katika umri wowote, lakini hutokea zaidi kwa watoto na hupotea yenyewe wanapofika umri wa kubalehe/kuvunja ungo, ingawa huweza kuendelea hata ukubwani.

Kwanini watu hutembea usingizini?

Sababu kuu ya kutembea usingizini haijulikani, ingawa inasemekana kuwa hali hii hurithishwa katika familia. Baadhi ya hali zinazoweza kupelekea kutembea usingizini ni:

 • Kutopata usingizi wa kutosha
 • Msongo wa mawazo
 • Homa kali (hasa kwa watoto)
 • Kunywa pombe kupita kiasi
 • Kutumia madawa ya kulevya
 • Kushtushwa na kelele za ghafla au mguso unaopelekea uamke kwa ghafla
 • Kuamka ghafla kutoka kwenye usingizi mzito ili kwenda chooni.

Nini cha kufanya kwa mtu anayetembea usingizini?

 • Hakikisha usalama wake. Jitahidi kumuongoza kurudi kitandani bila kujiumiza. Kwa kawaida, atarudi kulala.
 • Kumwamsha mtu baada ya kumlaza kitandani husaidia kuzuia hii hali kujirudia tena usiku huohuo.
 • Usipige kelele, kumshtua au kumkamata kwa nguvu, isipokuwa kama yupo kwenye hatari.
 • Hakikisha vitu hatarishi vimewekwa mbali mf vitu vyenye ncha kali, viberiti au vitu vinavyoweza kufanya ajikwae.
 • Kama muathirika hutembea usingizini katika muda uleule kila usiku, muamshe dakika 15-30 kabla ya muda huo. Hii husaidia kuzuia hali hii kwa kuvuruga mzunguko wa usingizi wa mwili.

Ushauri kwa anayetembea usingizini

Hakuna tiba maalum ya hali hii, lakini inasaidia kulala kwa muda wa kutosha.

 • Jenga mazoea ya kulala katika muda uleule kila usiku
 • Hakikisha chumba unacholala kipo kimya na taa zimezimwa
 • Punguza kunywa vinywaji vyovyote kabla ya kulala hasa vile vyenye kemikali ya โ€œcaffeineโ€ kama chai na kahawa. Nenda chooni kabla ya kulala
 • Tafuta njia ya kupumzika (relax) kabla ya kulala mfano kuoga maji ya uvuguvugu, kusoma au kuhema kwa nguvu (deep breathing)

Muda gani unapaswa kumuona daktari?

Mara nyingi hali hii haiihitaji utatuzi wa kitaalamu kwa kuwa huisha yenyewe au kupungua polepole kadri muda unavyoenda, hasa kwa watoto.

Muone daktari kama:

 • Hali hii hutokea mara kwa mara
 • Humzuia muathirika kupata usingizi wa kutosha
 • Huamka akiwa amechoka sana
 • Kama muathirika huwa katika hatari
 • Kama hali hii hujitokeza au kuendelea mpaka ukubwani.

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Privacy Preference Center