Tetekuwanga kwa watoto (Chicken Pox)

Ugonjwa wa tetekuwanga mara nyingi huathiri watoto, ingawa huweza kumuathiri mtu katika umri wowote. Husababishwa na kirusi cha “Varicella Zoster”. Kwa kawaida ni ugonjwa unaodhibitika ingawa huweza kuwa hatari kwa mtoto mchanga, mtu mzima au yeyote mwenye upungufu wa kinga mwilini. Karibu tujifunze zaidi kuhusu ugonjwa huu.

Je, ni rahisi kiasi gani kupata ugonjwa huu?
Tetekuanga huambukizwa kwa njia ya hewa baada ya mgonjwa kukohoa au kupiga chafya. Hivyo hata kuwa katika chumba kimoja na mgonjwa humweka mtoto katika hatari ya kuambukizwa.
Pia huambukizwa kwa kugusana na mtu mwenye ugonjwa huu au kushika vitu vilivyogusana na mgonjwa kama vile nguo au mashuka. Hii ni kama vitu hivi vina unyevuunyevu kutoka kwenye vidonda vya tetekuwanga

Ni kwa muda gani ugonjwa huu unaambukiza?
Tetekuwanga huanza kuambukiza kuanzia siku 2 kabla vipele havijaanza kutokea, mpaka vinavyokauka kabisa. Kwa kawaida ni siku 5 baada ya kuanza kutokeza.

Baada ya kuambukizwa, dalili huanza kuonekana baada ya muda gani?
Huchukua kati ya wiki 1 hadi 3 kutoka maambukizi mpaka vipele kuanza kutokea.

Dalili zake zikoje?


Kwanza, vipele vidogo vyekundu huanza kujitokeza sehemu yoyote ya mwili. Mara nyingi huanzia kifuani, usoni au mgongoni na kisha kusambaa mwilini kote.
Vipele hivi hujaa majimaji na baadhi huweza kupasuka. Huweza kusambaa au kubaki sehemu fulani ya mwili.
Baada ya kupasuka, huanza kukauka na kuacha mabakamabaka. Wakati huu, vipele vingine huanza kujitokeza sehemu nyingine za mwili.

Dalili zingine ni:
– Homa kali
– Maumivu ya mwili
– Kukosa hamu ya kula
– Kuwashwa sana

Nini cha kufanya kwa mtoto anayeugua

– Hakikisha anakunywa maji ya kutosha au vinywaji kama juisi ili kuweka mwili katika hali ya kutokukauka (dehydration).

– Mpe dawa za kutuliza maumivu.

– Mvalishe soksi mikononi kuepusha kujiumiza anapojikuna.

– Kata kucha za mikononi. Hii ni kuepusha kujikwaruza wakati anajikuna. Kumbuka kuwa kadri mtoto anavyojikuna vipele, ndivyo ambavyo vitaacha mabaka mabaya zaidi baada ya kupona.

– Mpake lotion au mafuta maalum ya kupuuguza mwasho.

– Muogeshe maji ya baridi kiasi kisha mkaushe kwa kupangusa polepole, na si kwa kufuta.

Nini cha kutokufanya kwa mtoto anayeugua

– Usimpatie dawa yeyote bila kupata ushauri wa mtaalam wa afya.

– Usimpatie dawa ya aspirin, hasa kama ana umri chini ya miaka 16. Hii huweza kusababisha ugonjwa wa “Rayes Syndrome” unaoshambulia ubongo na ini.

– Usimweke mtoto karibu na mama mjamzito, mtoto mchanga au mtu mwenye upungufu wa kinga mwilini mfano mgonjwa wa UKIMWI, kifua kikuu nk. Ugonjwa huu huwa ni hatari zaidi kwao.

– Kama mtoto ana homa, usimkande na maji ya baridi. Hii husababisha mishipa ya damu iliyo chini ya ngozi kusinyaa na hivyo kupelekea joto lililo ndani ya mwili kushindwa kutolewa nje. Hii huongeza joto mwilini na kufanya homa iwe kali zaidi.

Ni vyema tufahamu pia, kuwa ugonjwa wa Ukanda wa jeshi (Shingles) husababishwa na kirusi hikihiki kinachosababisha tetekuwanga. Baada ya kuingia mwilini, huweza kukaa ndani ya mwili kwa muda mrefu na miaka mingi badae (zaidi ya miaka 20) huleta ugonjwa huu wa Ukanda wa jeshi, hasa kinga ya mwili inapopungua. Hii huweza kuchochewa na msongo wa mawazo, baadhi ya magonjwa mfano UKIMWI na kifua kikuu, au tiba ya saratani ya madawa (chemotherapy)

Aidha, tafuta ushauri wa daktari, uonapo dalili zinazidi kuwa mbaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Top Posts & Pages

Recent Comments

CATEGORIES

Ratiba ya Wiki Hii

Jumatatu: Afya ya mtoto
Jumanne: Magonjwa yasiyo ya kuambukiza
Jumatano: Magonjwa ya Dharura na Magonjwa mengine
Alhamisi: Lishe na Mazoezi
Ijumaa: Ujauzito na Magonjwa ya Wanawake
Jumamosi: Afya ya uzazi
Jumapili: Magonjwa ya kuambukiza

POST REVIEWERS

Afya ya mtoto: Dr. Julieth Joseph
Afya ya Kinywa na Meno: Dr. Baraka Kileo
Famasia: Pharm. Hans Nniko
Sexual Health Dr. Deogratius Mtei
Lishe na Mazoezi: Dr. James Hellar
Magonjwa ya Dharura: Dr. Kilalo Mjema
Magonjwa ya moyo na Shinikizo la damu: Dr Hussein Manji
Saratani: Dr. Mathew Cosmas
Ujauzito na Magonjwa ya Wanawake: Dr. Walter Msirikale

About Us

Daktari Mkononi is a platform that contains health related information and connects health personnels and the society. Made by a group of medical students and overseen by doctors with love and passion to ensure healthy lives 🙂

CONTACT

Email:
daktarimkononi@gmail.com

SMS:
+255684159117
+255768256424

Whatsapp:
+255688636717

Subscribe

Tuandikie email yako tukutumie mada mbali mbali za afya uzipendazo.

Recent Posts

Upcoming Event

Homa ya Kichaa cha Mbwa | 28th September

Upcoming Show