Fahamu kuhusu magonjwa ya moyo yanayoweza kusababisha kifo cha ghafla

Kuna vifo ambavyo huibua mijadala sana katika jamii kwa mfano vifo vya wanariadha , wachezaji wa mpira wa miguu uwanjani na hata michezo mingine, je tatizo huwa ni nini?

Kifo cha ghafla kinachotokana na ugonjwa wa moyo ni kifo ambacho kinatokea ndani ya saa moja tangu dalili za ugonjwa zianze na inaweza tokea kwa mtu ambaye anajulikana kuwa ana ugonjwa wa moyo tayari au asiyejulikana kuwa na ugonjwa wa moyo.

Hali hii hutokea pale moyo unapoacha kufanya kazi ghafla hivyo basi hupelekea kukosekana kwa oksijeni katika sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo ubongo.

Sababu kubwa ya moyo kuacha kufanya kazi ghafla huwa ni pale moyo unapokuwa na mapigo yasiyo na mpangilio maalum (Arrhythmia), lakini kuna magonjwa ambayo yanapelekea moyo kuwa na mapigo haya, magonjwa hayo ni kama yafuatayo

-Mshtuko wa moyo

-Matatizo katika mishipa ya damu ya moyo

-Moyo kutanuka na kuwa mkubwa

-Kuta za moyo kupanuka

-Magonjwa ya valvu za moyo

-Hitilafu ya moyo ya kuzaliwa nayo

-Hitilafu katika uzalishaji na usafirishaji wa umeme katika moyo

Ni dalili zipi ambazo huashiria moyo kuacha kufanya kazi?

-Kama imetokea ghafla mtu huanguka, hupoteza fahamu na kushindwa kupumua papo hapo.

-Kama inatokea taratibu mtu hupata dalili kama vile maumivu ya kifua,  kuchoka kirahisi, mapigo ya moyo kwenda mbio n.k

Sababu hatarishi za kupata matatizo haya ni zipi?

Sababu ambazo zinaweza sababisha moyo kuacha kufanya ghafla ni;

-Historia ya kifamilia ya mtu kupoteza maisha ghafla au kuwa na magonjwa ya moyo

-Shinikizo la damu

-Kisukari

-Mafuta mengi mwilini

-Uvutaji sigara

-Unywaji pombe kuzidi kiasi

Je tatizo hili linazuilikaje?

Ili kulinda afya ya moyo na kupunguza uwezekano wa kupata hali hii ni vyema kuishi kwa kuzingatia kanuni za  afya ya moyo kwa kupunguza sababu hatarishi kwa kuzingatia yafuatayo; Kuacha uvutaji sigara, kunywa pombe kistaarabu na kufanya mazoezi, pia bila kusahau kufanya vipimo vya magonjwa ya moyo (checkups).

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Privacy Preference Center