TATIZO LA MTOTO WA JICHO KWA MTOTO(CATARACT)

 1. Mtoto wa jicho au cataract ni ukungu mweupe unaoonekena katika lensi ya jicho ambao unaweza kusababisha kuona kwa uhafifu au kupelekea upofu. Mtoto wa jicho ni moja kati ya sababu kuu zinazoweza kupelekea upofu kwa watoto waliozaliwa na tatizo hilo. Takwimu zinaonyesha kuwa mtoto wa jicho ni sababu kuu inayosababisha upofu duniani.

SABABU HATARISHI ZINAZOWEZA KUPELEKEA MTOTO KUZALIWA NA TATIZO HILI;

Sababu hizi zimegawanyika katika sehemu kuu mbili; za upande wa mama na upande wa mtoto

Sababu za upande wa mama ni kama zifuatazo;

 • Mama kuwa na lishe duni kipindi cha ujauzito
 • Mama kuwa na maambukizi ya virusi vya aina ya Rubela, na hii hupelekea mtoto kuzaliwa na tatizo la mtoto wa jicho, mtoto kuwa kiziwi, na kuzaliwa na tundu kwenye moyo
 • Mama kutumia dawa aina ya corticosteroids kipindi cha ujauzito
 • Mama kutibiwa kwa njia ya mionzi kipindi cha ujauzito

Sababu za upande wa mtoto;

 • Mtoto kukosa oxygeni ya kutosha wakati wa kuzaliwa kutokana na mama kutokwa damu nyingi wakati wa kujifungua
 • Mtoto kuwa na lishe duni kipindi cha mwaka wa kwanza baada ya kuzaliwa.

DALILI ZA MTOTO WA JICHO(CATARACT)

 • Kuonekana kwa ukungu mweupe kwenye sehemu ya katikati ya jicho la mtoto. Linaweza likawa moja au yote mawili. Hii ndio dalili ya kwanza aionayo mzazi.
 • Mtoto kushindwa kuona vizuri, kitu ambacho hugunduliwa na mama wa mtoto
 • Macho kuwa na makengeza
 • Sehemu nyeusi ya jicho kuwa inachezacheza

TIBA

 • Tiba pekee ya mtoto wa jicho ni upasuaji kuondoa lensi ya jicho iliyo na ukungu mweupe na kupandikizwa nyingine. Kama mtoto hajafikisha umri wa kupandikizwa lensi nyingine(miaka miwili), mtoto hupewa miwani kumuwezesha kuona na pia kulipa jicho zoezi ili lisiweze kupoteza uwezo wa kuona kwa sababu sehemu inayohusika na kuona bado haijakomaa.

Sio kila mtoto wa jicho huleta shida katika kuona ila ukungu uliopo katikati ya lensi unaozuia mwanga wenye taswira unaoweza kupenya na kufika katika sehemu inayohusika na kusafirisha mwanga kwenye ubongo iitwayo retina na hivyo hupelekea hitilafu katika uonaji. Kama ukungu huo ni mdogo na upo pembezoni mwa lensi na sio katikati hauwezi kupelekea uonaji hafifu au upofu.

Muwahishe mtoto hospitalini mapema mara baada ya kuona dalili moja wapo kwa sababu isipotibiwa kwa wakati mtoto anaweza kupoteza moja kwa moja uwezo wake wa kuona. Ni muhimu kwa mtoto kufanyiwa uchunguzi wa kina kwa sababu ukungu mweupe katika jicho kwa mtoto inaweza kusababishwa na kansa ya jicho ambayo hupelekea kifo isipogundulika mapema.