Mambo ya kuzingatia kabla ya kubeba ujauzito.

Jamii nyingi za kiafrika, swala la kubeba ujauzito huwa mara nyingi hutokea bila walengwa hasa wanawake kuwa wamejitayarisha, hivyo basi kupelekea kuwa na matatizo mengi kipindi cha ujauzito kwani hakukuwa na maandalizi yoyote juu ya ujauzito huo. Hivyo basi kama mwanamke yupo katika umri wa kuweza kubeba ujauzito au anapanga kupata ujauzito basi hivi ni baadhi ya vitu anatakiwa kuzingatia kabla ya kupata ujauzito ili kuweza kuwa na ujauzito salama na kujifungua mtoto mwenye afya nzuri bila matatizo yoyote.

1. Panga kukutana na mtaalam wa afya ya wanawake na ujauzito

Ni vyema kabla hujaamua kubeba ujauzito kakutana na mtaalam wa afya ya wanawake na ujauzito ambaye atakuchunguza kujua afya yako na historia ya familia yako na kukupa ushauri juu ya mambo ambayo unahitaji kufanya kabla ya kubeba ujauzito kama aina za dawa unazotakiwa kutumia au kutotumia wakati wa ujauzito, pia kupima maambukizi ili kuweza kukupatiwa tiba sahihi kabla ya kubeba ujauzito kwani magonjwa mengine huweza kuwa na adhari juu ya afya ya mtoto wako, mfano magonjwa kama kaswende, UKIMWI na rubella huweza kuambukizwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtotto aliyeko tumboni. Pia kupata ushauri juu ya magonjwa ya kurithi ambapo wewe na mwenzi wako mtapewa ushauri na kuchunguzwa viini saba ili kuweza kujua kama mmoja au wote mna magonjwa ya kurithi kama sickle cell anemia kabla ya kuamua kubeba mimba.

2. Meza vidonge vya folic acid

Ni kawaida sana kwa wengi kuanza kutumia vidonge vya folic acid wakati wanapoanza maudhurio ya kliniki za wajawazito lakini ni vizuri kuanza kutumia vidonge hivi hata kabla ya kubeba ujauzito ili kuweza kutengeneza akiba ya kutosha mwilini kabla ya kubeba ujauzito na kuendelea navyo wakati wa ujauzito. Hii husaidia sana katika kuzuia uwezekano wa  kupata mtoto mwenye mgongo wazi (neural tube defect) kwa asiimia 50 mpaka 70. Pia kula vyakula vyenye folic acid nyingi kama spinachi na jamii ya kunde.

3. Acha unywaji pombe na kuvuta sigara

Kama ni mtumiaji wa pombe au sigara , unashauriwa kuacha kutumia vilevi hivi kwani vina madhara kwako kama mama na kwa afya na mtoto wako. Tafiti nyingi zinaonyesha uvutaji wa sigara na unywaji pombe hupelekea mimba kuharibika, kuzaa kabla ya wakati(premature birth) na kuzaa watoto wenye uzito pungufu. Pia kuna uwezekano wa kuweza kupata mtoto mwenye ulemavu yaani “fetal- alcohol syndrome”, hivyo basin i vyema kuepuka utumiaji wa pombe na uvutaji wa sigara.

4. Kula mlo ulio kamili

Kipindi cha ujauzto mwili huongeza mahitaji yake ya chakula na nguvu, hivyo kabla ya kubeba ujauzito ni vyema ukawa uko katika hali nzuri kiafya ili kuweza kukidhi mahitaji ya mwili kipindi cha ujauzito, hivyo basi inashauriwa kula mlo uliokamilika wenye matunda na mbogamboga za kutosha ili kuweza kupata vitamini na madini muhimu mwilini ambayo huhitajika katika ukuaji mzuri wa mtoto aliye tumboni na pia kumkinga mama na mtoto na maradhi mbalimbali yatokanayo na upungufu wa lishe kama upungufu wa damu kipindi cha ujauzito ambayo huwa na madhara makubwa hasa wakati wa kujifungua.

5. Fanya mazoezi ya kuweka mwili imara

Mazoezi ni muhimu kwa kuwa na afya nzuri kwani husaidia kuwa na uzito sahihi kabla ya kubeba ujauzito. Kuwa na uzito pungufu au zaidi ni hatari hasa ukiwa mjamzito kwani huongeza nafasi ya kupata matatizo kipindi cha ujauzito. Uzito pungufu hupelekea mimba kuharibika na kuzaa mtoto mwenye uzito pungufu, huku uzito zaidi hupelekea kuweza kupata presha ya juu ya damu ambayo inaweza kupelekea kupata kifafa cha mimba. Hivyo basi kufanya mazoezi na kuweka mwili imara ni kitu cha msingi ca kuzingatia kabla ya kubeba ujauzito.

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Privacy Preference Center