Je, kuna madhara yoyote kwa mtoto ukijamiiana wakati wa ujauzito ?

Binadamu na baadhi ya viumbe vyenye vinasaba vinavokaribia sana kuafanana na vya binadamu kama samaki aina ya Dolphin ndio pekee wenye uwezo wa kujamiiana kwa lengo la kujifurahisha tu. Ingawa njia kuu ya kupata ujauzito ni kwa kujamiiana, maswali mengi hujitokeza iwapo kujamiiana wakati wa ujauzito kunaweza kuwa na athari kwa mtoto na hata juu ya usalama wa mimba kwa ujumla. Ukweli ni kwamba hakuna madhara yoyote yanayoweza kusababishwa na kujamiiana iwapo mimba inakua katika hali ya kawaida kiafya.

Pamoja na hayo, maswali mengine hayaepukiki. Je, kujamiiana kunaweza kusababisha mimba kutoka (Miscarriage) ?.

Hapana, mimba inaweza kutoka iwapo kuna matatizo katika ukuaji wa mtoto tumboni. Lakini kama mtoto anakua vizuri tumboni, kujamiiana hakuwezi kusababisha mimba kutoka.

Je, kujamiiana kunaweza kumdhuru mtoto akiwa tumboni ?.

Hapana, kijusi kinalindwa na mfuko wa uzazi, maji ya uzazi ambayo hunyonya mikandamizo isimfikie kijusi na hata misuli minene ya kuta za mji wa mimba. Isipokuwa kwa usalama zaidi ni vema kuepuka mikao itakayo kandamiza tumbo au ambayo itasababisha mimba kuelemea upande wa nyuma (chali) hali inayoweza kuziba mishipa mikuu ya damu inayopita kwa nyuma ya mji wa mimba.

Je, kujamiiana kunaweza kusababisha uchungu kabla ya muda wake ?.

Uchunguzi umeonesha kwamba shahawa kutoka kwa mwanaume zina kemikali zinazoitwa prostaglandins ambazo zinaweza kusisimua kuta za mji wa mimba kukaza lakini sio kwa kiwango cha kusababisha uchungu kabla ya wakati wake. Aidha, kufika kileleni kwa mwanamke kunaweza kusababisha kukaza kwa kuta za mji wa mimba ingawa kwa kiwango kidogo kisichoweza kusababisha uchungu. Isipokuwa, kwa mwanamke mwenye historia ya kupata uchungu kabla ya wakati anaweza akashauriwa na daktari wake asijihusishe na kujamiiana.

Kwa upande mwingine kuna mambo kadha wa kadha yanayoweza kumfanya daktari akashauri mwanamke asijihusishe na kujamiiana kama vile:

  • Iwapo mjamzito anavuja damu ukeni bila sababu.
  • Iwapo maji ya uzazi yanavuja.
  • Iwapo mlango wa uzazi (cervix) umefunguka kabla ya wakati.
  • Iwapo Plasenta imefunika mlango wa uzazi (Placenta previa).
  • Iwapo mjamzito ana historia ya kupata uchungu au kujifungua kabla ya wakati.
  • Iwapo mjamzito anabeba mapacha.

Vile vile, ni muhimu kumkinga mtoto aliyeko tumboni dhidi ya magonjwa yanayoweza kuambukizwa kwa njia ya kujamiiana. Pamoja na ulinzi mkali anaoupata mtoto tumboni, vijidudu vya magonjwa ya zinaa kama vile UKIMWI, Kaswende na kisonono vinaweza kupenya na kumdhuru mtoto. Ni hatari kujamiiana na mwenza wako iwapo amegundulika hivi karibuni na ugonjwa wowote wa zinaa.

Kumbuka, daktari anapokushauri usijamiiane wakati wa ujauzito, anamaanisha usijihusishe na kitu chochote kinachoweza kukusisimua kingono sio tu kuingiliana kimwili.

Privacy Preference Center