Nimepata mapacha wenye baba tofauti, imewezekanaje ? (Heteropartenal superfecundation) Sehemu A

Kabla hujasema kitu hakiwezekani kumbuka, “asili haisomi vitabu”. Ni ajabu lakini kweli, mapacha wanaweza kuwa na baba tofauti hali inayofahamika kitaalamu kama Heteropartenal superfecundation. Ingawa ni jambo la kawaida sana kwa mamalia wengine kama Paka, kwa binadamu mapacha wenye baba tofauti hutokea mara chache sana. Katika uchunguzi uliowahi kufanyika, katika mapacha wasiofanana 39,000, mapacha watatu (3) walikua ni mapacha wenye baba tofauti.

Mapacha wenye baba tofauti wanaweza kupatikana kwa njia kama tatu ambazo ni;

  1. Iwapo mayai mawili yatapevushwa katika mzunguko mmoja
  2. Iwapo mwanamke ana miji miwili ya mimba (Uterus didelphys)
  3. Urutubishaji kwa njia isiyo ya asili (artificial insemination)

Kwa hali ya kawaida, mwanamke hupevusha yai moja kila mwezi katika moja ya ovari mbili alizonazo. Kisha, huliachilia yai hilo kuelekea kwenye mji wa mimba kwa ajili ya urutubishaji kutoka kwa mbegu za kiume. Mara tu baada ya yai kurutubishwa, mimba hutungwa na shughuli za ovari kupevusha mayai husimama mpaka mtoto atakapozaliwa.

Wakati mwingine,mayai mawili yanaweza kupevushwa katika kila ovari na kuachiliwa kwa wakati mmoja. Iwapo mayai hayo yatarutubishwa, mimba ya mapacha wasiofanana inaweza kutungwa. Hii ni tofauti na mimba ya mapacha wanaofanana ambapo yai moja la mwanamke hurutubishwa na yai moja la mwanaume na kisha yai hilo kugawanyika na kutengeneza vijusi viwili.

Pia, yai la mwanamke huweza kukaa hadi masaa 48 bila kuharibika likisubiri kurutubishwa. Vile vile, mbegu za kiume huweza kudumu siku 3 hadi 5 zikisubiri kurutubisha yai mara tu likipevuka.

Hivyo, Iwapo mwanamke atajamiiana na wanaume wawili tofauti katika kipindi cha siku 3 mpaka 5 kabla ya upevushaji wa mayai (ovulation), na iwapo mwanamke huyo atapevusha mayai mawili katika ovari zote mbili kwa wakati mmoja, mimba ya mapacha wenye baba tofauti inaweza kutengenezwa.Hii ni tofauti na hali nyingine inayofahamika kama superfetation ambapo vijusi vinaweza vikatofautiana hadi wiki moja na zaidi. Hii hutokea mara chache zaidi kuliko mapacha wenye baba tofauti.

Katika makala yajayo tutazungumzia ni jinsi gani mapacha wenye baba tofauti wanaweza kupatikana kwa njia zilizobaki.

2 thoughts on “Nimepata mapacha wenye baba tofauti, imewezekanaje ? (Heteropartenal superfecundation) Sehemu A

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Privacy Preference Center