Ninaweza kuwa na mwenzi aliyeathirika wakati mimi sijaathirika? (Discordant Couples)

Wapo baadhi ya wenzi
wenye mahusiano ya muda mrefu ambao kati yao mmoja ni muathirika wa virusi vya
ukimwi VVU, na mwingine si muathirika.

 

Kutokana na tafiti nyingi zilizofanyika, maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa watu walio kwenye ndoa, kwa sehemu kubwa ni matokeo ya kukosekana uaminifu kati yao, ambapo mmoja wao au wote, wanakuwa na mahusiano kimwili na mtu/watu wengine nje ya ndoa, maarufu kama michepuko. Sababu nyingine zinazoweza kupelekea maambukizi kama vile, kuongezewa damu yenye VVU, kuchangia vitu vyenye ncha kali, kurithi mume au mke, zipo lakini kwa sehemu ndogo sana.

Hatuwezi kukanusha ukweli kwamba mwenzi wako akiathirika, na wewe upo kwenye hatari kubwa zaidi ya kuwa muathirika.

Sasa je, ni kipi kinapelekea baadhi ya wenzi

kutofautiana kiafya, licha ya kujamiana pasipo kinga kwa muda mrefu na mwenzi aliye athirika na VVU?

Sababu moja au zaidi kati ya zifuatazo inahusika

·       Kutofautiana vinasaba (DNA) vinavyoratibu uwezekano wa mtu kuambukizwa VVU. Baadhi ya watu wana mabadiliko ya kijenetiki katika kinasaba cha CCR5 kinachoratibu uwezekano wa kuambukizwa VVU na hivyo kuwafanya kuwa sugu kwa virusi vya ukimwi, watu hawa hawashambuliwi na virusi vya ukimwi.

·       Aina ya kirusi cha ukimwi alichonacho mwenzi wako. Virusi vya ukimwi vipo vya aina nyingi lakini vimegawanyika katika makundi makubwa mawili HIV-1 na HIV-2, haya hutofautiana uwezo wa kushambulia na kuambukiza. HIV-2 ina uwezo mdogo wa kuambukiza, na makali yake ya ugonjwa ni madogo ukilinganisha na HIV-1. HIV-2 inapatikana sana Afrika ya magharibi.

·       Kiwango cha maambukizi aliyo nayo mwenzi aliyeathirika na uimara wa kinga yake ya mwili. Iwapo maambukizi yapo katika hatua za awali, idadi ya virusi mwilini si kubwa na kinga ya mwili haijazidiwa bado, uwezekano wa kuambukizwa VVU unapungua kwa asilimia kubwa.

·       Magonjwa mengine ya zinaa, uwepo wa magonjwa mengine ya zinaa unarahisisha kusambaa kwa virusi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwani yanaharibu njia za asili zinazomlinda mtu asipate maambukizi. Magonjwa haya yasipokuwepo uwezekano wa kusambaza VVU unapungua.

Sambamba na yote yaliyoelezwa hapo juu, kuna umuhimu mkubwa wa kila mtu kupima afya yake ili atambue hali yake. Hii itawasaidia wenzi kujilinda zaidi ili kudumisha furaha katika mahusiano yao. Iwapo mmoja atakuwa ameathirika na mwingine bado, mnashauriwa kufika kituo cha afya kwa ajili ya ushauri zaidi kujua namna ya kuendeleza mahusiano yenu licha ya kutofautiana kiafya.

Iwapo matumizi ya dawa za kupunguza VVU, lishe bora, mazoezi, mtazamo chanya wa maisha, upendo, na matumizi ya kinga kwa mwenzi aliyeathirika vitazingatiwa kwa ufasaha. Tunaweza kuitunza furaha ya mahusiano yetu na kuwakinga wenzi wetu dhidi ya maambukizi.

Lakini! Kwa nini tusubiri kujenga ukuta wakati tunaweza kuuziba ufa uliopo?? Kanuni ya msingi ni kuwa mwaminifu inaanza na wewe (it begins with you!)

3 thoughts on “Ninaweza kuwa na mwenzi aliyeathirika wakati mimi sijaathirika? (Discordant Couples)

  1. safi sana kwa Maelezo dk magomele,lakini napenda kidogo kwenye HIV testing uongezee kuhusu vipimo HIV SD bioline na unigold kwasababu kuna sintofahamu nyingi hutokea katika utoaji wa majibu

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Privacy Preference Center