Lishe kwa mtoto mwenye maambukizi ya virusi vya ukimwi (Sehemu A)

Lishe bora ni muhimu kwa watoto wote hususani wenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa ajili ya ukuaji na maendeleo yao.Watoto wanaoishina virusi vya UKIMWI na wenye UKIMWI wako katika hatari kubwa ya kupata utapiamlo kutokana na ;

 • Maradhi ya mara kwa mara.
 • Ongezeko la mahitaji ya virutubishi hasa nishati-lishe.
 • Ulaji duni
 • Uyeyushwaji na ufynzwaji duni wa virutubishi mwilini

Mengi ya maradhi yaambatishwanayo na kuishi na virusi vya UKIMWI na Ukimwi huathiri mfumo mzima wa ulaji wa chakula na kusababisha lishe duni. Lishe duni hudhoofisha mfumo wa kinga, hivyo mtoto hua katika hatari kubwa ya kupata maradhi mbalimbali kwa urahisi.

Watoto walio chini ya miaka mitano huwa na kawaida ya kupelekwa kliniki ili kufuatilia maendeleo yao ya ukuaji na afya kwa ujumla. Swali kuu ni, “Vipi kuhusu watoto waliovuka miaka mitano? ” Hali imekua mbaya zaidi kwa watoto walio katika umri wa miaka 6 hadi 9 kwani hawana mfumo wa ufuatiliji wa maendeleo yao yao ya ukuaji na afya, inayopelekea ukosekanaji wa huduma muhimu ikiwemo taarifa kuhusu lishe bora.

 

Athari za virusi vya UKIMWI kwenye hali ya lishe ya mtoto.

Kuna athari  mbali mbali zisababishwazo na virusi vya UKIMWI ambazo humuweka mtoto katika hatari ya kupata utapiamlo. Athari hizo ni pamoja na;

 1. Ongezeko la mahitaji ya virutubishi mwilini.

Mtoto mwenye virusi vya UKIMWI huhitaji nishati-lishe kwa wingi ukilinganisha na mtoto asiye na virusi hivyo. Hii ni sababu ya ongezeko la matumizi ya nishati-lishe mwilini kutokana na;

 • Upunguaji wa uwezo wa mtoto kula chakula, uyeyushwaji wa chakula na ufyonzwaji pungufu wa virutubishi.
 • Mabadiliko katika umetaboli(ujenzi na uvunjaji wa kemikali mwilini)

    2. Mwili kushindwa kutumia baadhi ya virutubishi.

Virusi vya UKIMWI husababisha mwili kushindwa kutumia baadhi ya virutubisho kama vile protini, mafuta  na wanga kikamilifu.

   3. Ulaji duni.

Mtoto mwenye virusi vya UKIMWI hukosa hamu ya kula. Hali hii husababisha mtoto kushindwa kuka chakula cha kutosha au kukataa kula kabisa kutokana na matatizo ya kuwa na vidonda vinywani au kooni.

   4. Kutapika au kuharisha.

Hali hii husababisha upotezaji wa virutubishi kutoka katika mwili wa mtoto,kwani chakula hakikai tumboni kwa muda wa kutosha ili kuyeyushwa na virutubishi kufyonzwa.

Mahitaji ya chakula na lishe kwa mtoto mwenye virusi vya UKIMWI

Kuna umuhimu kwa mtoto yeyote kupata chakula mhanganyiko na cha kutosha ili kukidhi mahitaji ya mwili. Mahitaji yanishati-lishe kwa mtoto mwenye virusi vya UKIMWI asiye nadalili za UKIMWI huongezeka kwa asilimia 10. Mtoto mwenye dalili za UKIMWI bila kupungua uzito, mahitaji yake ya nishatilishe huongezeka kwa asilimia 20 hadi 30. Kwa mtoto mwenye dalili za UKIMWI na anayepungua uzito, mahitaji huongezeka kwa asilimia 50 hadi 100 zaidi ya kiasi cha kawaida. Kutokana na hayo, mtoto mwenye virusi vya UKIMWI anahitaji kuongezewa kiasi cha chakula, idadi ya milo kwa siku na aina za vyakula anavyokula katika kila mlo.

Yafuatayo ni makundi ya vyakula yanayounda mlo kamili;

A. Vyakula vya nafaka, mizizi na ndizi.

Hivi huchukua sehemu kubwa ya mlo na kwa kawaida ndivyo vyakula vikuu. Vyakula katika kundi hili ni pamoja na mahindi, mchele, mtama, ulezi, viazi vitamu, viazi vikuu, mihogo, ndizi navyote vya jamii hiyo.

B. Vyakula vya asili ya nyama na jimii ya kunde.

Kundi hili limegawanyika katika sehemu mbili.
(a) Vyakula vyenye asili ya wanyama

Kama vile nyama, samaki, dagaa, maziwa, kuku, mayai, jibini, maini, figo, na wadudu wanaoliwa kama senene, nzige, na kumbikumbi.

(b) Vyakula vya jamii ya kunde
Kama vile maharagwe, njegere, kunde, karanga, soya, njugu mawe, dengu, choroko na fiwi.

C. Mboga-mboga

Kundi hili linajumuisha aina zote za mboga-mboga kama vile mchicha, majani ya maboga, kisamvu, majani ya kunde, matembele, spinachi, mnafu, mlenda, karoti, pilipili hoho, biringanya, matango, maboga, nyanya chungu, kabichi na figiri.

D. Matunda

Kundi hili linajumuisha matunda ya aina zote kama vile papai, embe, pera, limau, ndimu, pasheni, nanasi, peasi, chungwa, chenza, zambarau, fenesi, stafeli, bungo, pichesi, topetope.

E.Mafuta

Mafuta ni muhimu kwa afya ingawa yanahitajika kwa kiasi kidogo tu mwilini. Mafuta hupatikana kwenye mbegu mbalimbali zitoazo mafuta kama vile alizeti, ufuta, karanga, mawese, kweme na pamba. Mafuta mengine ni pamoja na siagi, samli na nyama za mafuta.

Maji hayahesabiwi kama kundi la chakula, lakini ni muhimu sana katika kuyeyusha chakula na kusafirisha virutubishi mwilini. Ili kukidhi mahitaji ya maji mwilini, inashauriwa mtoto anywe maji ya kutosha kila siku. Inashauriwa anywe
maji mengi zaidi wakati wa joto kali ili kuzuia upungufu wa maji mwilini. Vilevile mtoto anaweza kuongeza maji mwilini kwa kunywa vinywaji kama madafu, au juisi ya matunda mbalimbali.

 

Umuhimu wa lishe bora kwa mtoto mwenye virusi vya UKIMWI

Ni muhimu mtoto mwenye maambukizi ya virusi vya ukimwi kuwa na lishe bora ili;

 1. Kuboresha kinga ya mwili dhidi ya maradhi mbalimbali.
 2. Kukidhi ongezeko la mahitaji ya nishati-lishe na virutubishi mwili.
 3. Kuboresha ukuaji wa akili na mwili
 4. Kurudisha vitamini, madini na virutubishi vingine vinavyopotea kutokana na maradhi kama vile kuharisha na kutapika.
 5. Kumpa nguvu za kucheza na kufanya shughuli mbalimbali.
 6. Kumpa nguvu za kucheza na kufanya shughuli mbali mbali.
 7. Kusaidia dawa zinazotumika kufanya kazi kwa ufanisi mwilini.
 8. Kuboresha afya hivyo kuweza kurefusha kipindi cha kuishi.

Je,ni nini kifanyike ili kuboresha lishe kwa mtoto mwenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI?  Tukutane wiki ijayo katika muendelezo wa mada hii.

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Privacy Preference Center