Je, kuna madhara gani kufanya mapenzi kinyume na maumbile(anal sex)?

Pengine umewahi jiuliza swali kama hili ama umewahi sikia mtu mwingine akiuliza au pengine ni mara yako ya kwanza kukutana na swali hili, hilo lisikupe tabu hata kidogo mpenzi msomaji wetu wa makala zetu za afya ndani ya daktari mkononi kwani leo tutajifunza pamoja madhara yaambatanayo na kufanya mapenzi kinyume na maumbile, karibu sana.

Kufanya mapenzi kinyume na maumbile ni nini hasa?

Tunaposema kufanya mapenzi kinyume na maumbile tunamaanisha kufanya mapenzi kupitia njia ya haja kubwa badala ya uke.

Je, hili jambo lipo kwenye jamii yetu?

Ndani ya jamii yetu ya kitanzania kufanya mapenzi mapenzi kinyume na maumbile ni mwiko na jambo hili limekuwa likikemewa vikali na tamaduni zetu, dini na sheria za nchi. Lakini ni ukweli usiopingika kuwa kutokana na utandawazi jambo hiki tulilokuwa tunalisikia kwenye nchi za magharibi linazidi kukita mizizi kwenye jamii yetu. Pengine hii pia imechangiwa na udadisi wa kutaka kujaribu mambo mapya au pengine  kuigana miongoni mwa vijana wengi. Hivyo basi ni jambo la msingi kujifunza madhara ya aina hii ya ngono.

Madhara makuu ya kufanya mapenzi kinyume na maumbile.

Madhara ya ufanyaji mapenzi kinyume na maumbile yanatokana na utofauti wa asili baina ya njia ya haja kubwa na uke, njia ya haja kubwa siyo maalum kwa ajili ya shughuli ya kufanya mapenzi hivyo una muundo na asili tofauti kabisa na uke ambao ni maalum kwa shughuli hiyo. Hivyo basi madhara makubwa ni pamoja na:-

1.Maambukizi sugu ya njia ya mkojo (UTI).

Njia ya haja kubwa ina idadi kubwa ya aina mbalimbali za bakteria ambao hukua na kuzaliana katika eneo hili. Bakteria hawa huingia katika njia ya mkojo ya mwanaume wakati wa tendo, na baada yakuingia husababisha maambukizi katika njia ya mkojo. Pia wanawake hupata maambukizi haya sugu kutokana hasa na tabia ya kutoa uume  katika njia ya haja kubwa kuuingiza moja kwa moja kwenye uke wakati wa tendo,hii hupelekea usafirishaji wa bakteria hawa kutoka sehemu ya haja hadi kwenye njia ya mkojo ya mwanamke. Maambukizi haya huambatana na maumivu makali wakati wa kukojoa.

2.Michaniko na michubuko.

Kutokana na njia ya haja kubwa kukosa umajimaji uliopo katika uke kwa ajili ya kurahisisha muingiliano,kufanya mapenzi kwa njia ya haja kubwa hupelekea michubuko na michaniko ambayo huongeza maradufu hatari ya kupata magonjwa ya zinaa kama vile kaswende, kisonono, klamadia na HIV/AIDS.

3.Kulegea kwa misuli ya haja kubwa.

Misuli ya njia ya haja kubwa haina uwezo wa kutanuka na kujirudi kama ile ya uke. Hivyo kufanya mapenzi kwa njia ya haja kubwa hupelekea kulegea kwa misuli hii hivo kushindwa kufanya kazi zake za kawaida, hii hupelekea kupungua kwa uwezo wa kukaa na haja kubwa (fecal incontinence), pia hali hii inaweza leta ugumu kwa wanawake wajawazito wakati wa kujifungua linapokuja suala la kubana pumzi.

4.Saratani ya njia ya haja kubwa(colon cancer).

Pia kufanya mapenzi kwa njia huongeza hatari ya kupata saratani ya njia ya haja kubwa  ijulikanayo kitaalamu kama colon cancer.

5.Kuziba njia ya mkojo

Pia kutokana na uchafu uliopo katikq njia ya haja kubwa, uchafu huo unapoingia katika njia ya mkojo(urethra) huweza kupelekea kuziba kwa njia ya mkojo hivyo kupelekea maumivu na maambukizi katika mfumo wa mkojo.

6.Magonjwa ya kibofu na figo.

Hii hutokana na maambukizi sugu katika njia ya mkojo(UTI) baadaye hupelekea magonjwa ya kibofu kama vile uvimbe na saratani ya kibofu, pia maambukizi kwenye figo hupelekea figo kushindwa kufanya kazi hali ambayo huweza kupelekea kifo.

Ndugu mpenzi msomaji ni matumaini yangu kuwa umepata kitu katika makala ya siku ya leo, kama una swali ama dukuduku lolote timu ya daktari mkononi tunapenda kusema kwamba usisite kuwasiliana nasi kwani muda wote tupo kwa ajili yako wakati wowote katika simu ya kiganjani mwako. Tuonane tena wiki ijayo katika makala za afya ya uzazi hapahapa ndani ya daktari mkononi.

tembelea daktari mkononi kila siku kwa Makala motomoto za afya.


Erasto-Ipyana

Wherever the art of medicine is loved there's love of humanity.

All author posts

Privacy Preference Center