Fahamu kuhusu ukuaji wa mtoto wako.

Kila mtoto mwenye afya njema hufuata ukuaji maalumu ambao umefanyiwa utafiti kwamba unafuatwa na watoto wotekitaalamu kama “developmental milestone”. Ikitokea mtoto akakua aidha chini au juu ya ukuaji huu anaweza kua na tatizo hivyo basi anatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa haraka.

Hatua muhimu za ukuaji wa mtoto anapozaliwa hadi miaka mitatu

Ukuaji wa kimwili.

Kwa kawaida ukuaji wa mwili kwa mwaka wa kwanza huenda kwa kasi kubwa. Kasi hii hutegemea sana na ubora wa lishe, mazingira rafiki ya ukuaji, afya ya mwili na hata nasaba za ukuaji alizorithi mtoto kutoka kwa wazazi wake wawili. Baada ya kumaliza miezi sita, mtoto huanza kuota meno kwa mkupuo wa meno mawili mawili yakianzia kwenye ufizi wa chini na kisha ufizi wa juu. Ni wakati huo huo ambapo mtoto huanza kukaa mwenyewe hatua kwa hatua kisha ndani ya miezi 12 ya mwanzo huanza kutambaa, kusimama na hatimaye kuchukua hatua ya kwanza kabla au baada tu ya mwaka wa kwanza.
Kwa muda wote wa miaka mitatu ya mwanzo, kwa ujumla, mtoto huwa bado akijifunza kuvimudu viungo vya mwili wake na kuvitumia kwa usahihi ili aweze kukabiliana na changamoto za kimazingira. Kinywa ndiyo sehemu inayomsisimua mtoto katika kipindi hiki hivyo usafi na uangalizi wa karibu unahitajika vinginevyo anaweza kujikuta akipata magonjwa yatokanayo na uchafu.

Ukuaji wa kiakili.

Kiakili, mtoto huzaliwa na ubongo unaochemka vizuri ili kumwezesha kuyaelewa mazingira yake na hivyo kujenga kumbukumbu za mambo anayokutana nayo bila kutegemea mafundisho/maelekezo yoyote. Katika miezi sita ya mwanzo, mtoto huwa na shughuli kubwa ya kujenga uzoefu unaofanana na vipande vya filamu kulingana na watu na mazingira yamzungukayo. Hii ina maana kwamba anachofikiri mtoto huanzia kwenye kile kinachofanyika kwenye mazingira yake ikiwa ni pamoja na mwili wake mwenyewe. Ndani ya mwaka mmoja mtoto huweza kukumbuka uwepo wa vitu asivyoviona kwa macho kuthibitisha kwamba kumbukumbu yake inaimarika. Katika kipindi hiki, hujenga uwezo wa kutafuta vilivyofichwa pamoja na kutambua sauti za watu anaowafahamu wanaomzunguka. Tukio jingine muhimu la ukuaji wa kiakili ni matumizi ya lugha katika kuwasiliana na wanaomzunguka kati ya miezi 12 na 18. Mtoto huanza kutumia maneno katika kuwasiliana na wengine. Ongezeko la misamiati ni dalili ya ukuaji kwa akili na uelewa wa mtoto .

Visababishi vya ukuaji duni wa mtoto.

Kuna sababu mbalimbali ambazo hufanya mtoto ashindwe kukua kulingana na mfumo wa “developmental milestone”. Zifuatazo ni sababu zinazopelekea ukuaji duni wa mtoto;

a) Lishe duni

b) Magonjwa mbalimbali kama; magonjwa ya moyo, kuharisha,kisukari,kifua kikuu.

c) Matatizo ya kinga haswa yale ya kinga ya mwili.

d) Upungufu wa homoni za ukuaji maarufu kama “growth hormones”

Kadhalika uzalishwaji wa homoni za ukuaji kuliko kawaida humfanya mtoto kukua kuliko kawaida.

Utaratibu wa kwenda kliniki kwa muda wa miaka mitano umewekwa ili kuhakikisha ufuatiliwaji wa mtoto kwa ukaribu ili kuhakikisha maendeleo ya afya na ukuaji ya mtoto ili kama kuna tatizo lolote basi lifanyiwe kazi kwa wakati. Ni muhimu kuhudhuria kliniki hata kama ukiona mtoto amekua.Β 

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Privacy Preference Center