Nilikatwa mguu kwa sababu ya kisukari – Sehemu ya Pili

Soma sehemu ya kwanza kwa kubofya hapa 

Nilikatwa mguu kwa sababu ya kisukari

Je, kisukari kinaweza kuathiri miguu? Hakika; kisukari kinaweza kuathiri sehemu yoyote ya mwili!

Mtu mwenye kisukari huwa na kiwango cha sukari kilichopitiliza juu ya kiwango stahiki kwenye damu. Baada ya muda mrefu, hali hii huweza kupelekea kutokuwa na hisia yoyote mguuni. Waweza kujikwaa, kujikata au kuungua na usijue lolote!

Hali kama hii huleta vidonda vibaya mguuni vinavyoalika vijidudu vinavyosababisha ugonjwa kuingia mwilini. Hali hii ikiwa mbaya zaidi, waweza kulazimika kukatwa mguu! Mishipa ya damu inapoathiriwa hupelekea mguu kukosa damu ya kutosha; damu inayobeba virutubisho na oxygen. Hivyo, mgu huchukua muda mrefu zaidi kupona baada ya kuumia na kupata kidonda

Tambua dalili za mguu kuathiriwa na kisukari

Mojawapo ya dalili za kwanza ni unyevuunyevu au majimaji kwenye miguu inayoweza kuloanisha soksi au kuvuja kwenye kiatu.

Mguu kuvimba, kuwa mwekundu na kutoka harufu mbaya ni baadhi ya dalili za awali za hali hii

Kiashiria kikubwa cha hali hii kuwa mbaya ni kidonda kubadilika rangi na kuwa cheusi; na ngozi yenye kumenyeka kirahisi. Hii hutokana na mguu kukosa mzunguko wa damu katika sehemu hio ya mguu. Hii hufuatwa na majimaji kutoka na harufu mbaya, maumivu au kukosa hisia kabisa kwenye mguu

Dalili za mguu wa kisukari zaweza zisiwe dhahiri. Si ajabu kama mgonjwa wa kisukari haoneshi dalili zozote mpakak kidonda kinapovamiwa na vijidudu na kusababisha magonjwa

Sababu zinazopelekea kuoza kwa mguu kutokana na kisukari

 • Mzunguko hafifu wa damu
 • Kiwango cha sukari kuwa juu kwenye damu
 • Mishipa ya fahamu kwenda kwenye mguu kuathiriwa
 • Mguu kuumia na kusababisha vidonda
 • Ngozi kuwa kavu na kukatikakatika

Mishipa ya fahamu / neva huathiriwa baada ya muda mrefu. Dalili za kwanza ni kuhisi kuchomwachomwa kwenye mguu, mguu kuuma; na baada ya muda, hisia kwenye mguu hupungua kufikia kushindwa kuhisi chochote kwenye mguu!

Ni nani aliye katika hatari?

Mtu yeyote mwenye kisukari yupo katika hatari ya mguu kuoza, kama asipodhibiti kiwango cha sukari mwilini!

Aidha, yafuatayo huongeza hatari hii:

 • Kuvaa viatu vinavyobana au vinavyoumiza miguu
 • Kutosafisha miguu vizuri mara kwa mara
 • Kutokata kucha za miguu au kukata vibaya
 • Utumiaji wa pombe na sigara

 

 • Matatizo ya macho kutokana na kisukari
 • Magonjwa ya moyo au figo
 • Unene uliopitiliza

Jinsi ya kujikinga

Cha kwanza na cha muhimu kuliko yote ni kudhibiti kiwango cha sukari mwilini kwa kuzingatia maelekezo kutoka kwa mtaalamu wa afya. Pia zingatia usafi wa mwili hasa wa miguu

 • Kagua miguu kila siku
 • Safisha miguu vizuri kila siku
 • Weka ngozi ya miguu katika hali ya ulaini kwa kupaka mafuta
 • Kata kucha za miguu mara kwa mara
 • Vaa viatu vinavyokutosha. Vaa soksi wakati wowote kuepusha michubuko wakati wa kutembea. Badilisha soksi unazovaa kila siku
 • Epuka kuweka miguu katika hali ya baridi sana au joto sana

Kumbuka kuwa vidonda vya miguu vyaweza kurudi tena baada ya kupona. Hivyo, hakikisha unatembelea kituo cha afya mara kwa mara kwa ajili ya vipimo stahiki. 

Usipoteze mguu wako kwa kisukari!

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Privacy Preference Center