Umuhimu wa Vitamini aina ya ‘Asidi ya Foliki’ Kwa Mama Mjamzito.

Asidi ya foliki ni moja ya vitamini katika kundi la vitamini B. Asidi ya foliki (vitamini B9) pamoja na kazi nyingine, husaidia katika utengenezaji wa vinasaba (DNA) na hivyo seli za mwili.

Umuhimu wa asidi ya foliki kwa mama mjamzito, unaweza kugawanyika katika sehemu mbili; umuhimu kwa mama na umuhimu kwa mtoto.

UMUHIMU KWA MAMA.
i) Husaidia kupunguza shinikizo la juu la damu
ii) Pamoja na vitamini B12, asidi ya foliki, hupunguza uwezekano wa kuwa na upungufu wa damu (Anaemia)
iii) Tafiti zinaonesha kuwa, asidi ya foliki, hupunguza uwezekano wa kuugua saratani, kwa sababu huzuia mabadiliko ya vinasaba ambayo hupelekea saratani.
iv) Tafiti pia zinaeleza kuwa, asidi ya foliki, husaidia kupunguza hatari ya kujifungua kabla ya wakati (preterm delivery)

UMUHIMU KWA MTOTO.
Vitamini B9 (asidi ya foliki) hupunguza nafasi ya mtoto kupata na magonjwa ya kuzaliwa nayo (congenital diseases) kama vile
i) Mgongo wazi (spina bifida)
ii) Kichwa kikubwa (hydrocephalus)
iii) Matatizo ya moyo (congenital heart disease)
iv) Mdomo sungura (cleft palate)

NITAIPATA WAPI ASIDI YA FOLIKI?
Yamkini unajiuliza swali hili, asidi ya foliki hupatikana katika vyakula mbalimbali kama vile mboga za majani za kijani kama vile mchicha, matunda jamii ya michungwa, maharagwe makavu na kadhalika.
Tafiti zinaonesha kuwa vyakula hivyo havina asidi ya foliki ya kutosha kukidhi mahitaji ya mwili wakati wa ujauzito, hivyo ni vizuri kupata nyongeza ya vitamini hivi kwa kumeza vidonge. Hii huitwa lishe mbadala.

NI WAKATI GANI NIMEZE VIDONGE VYA ASIDI YA FOLIKI?
Asidi ya foliki huhitajika kwa kiwango kikubwa miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito. Lakini tafiti zinaonesha kuwa, uhitaji huwa mkubwa Zaidi siku 28 za kwanza tangu kutungwa kwa mimba. Hivyo huu ndio muda unaoshauriwa kumeza vidonge vya asidi ya foliki:-
• Msichana baada ya kuvunja ungo
• Mwanamke anaejiandaa kushika ujauzito
• Mama mjamzito pale anajigundua ni mjamzito.
Ikumbukwe kuwa kuchelewa kumeza vidonge vya asidi ya foliki, haitasaidia kupunguza madhara kwa mtoto hata kama mama ataanza kumeza.

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Privacy Preference Center