Kibiyongo, kwa kitaalamu ikijulikana kama ‘kyphosis’ ni kupinda kwa uti wa mgongo inayosababisha sehemu ya juu ya mgongo kuonekana duara zaidi kuliko kawaida. Kila mtu ana upindo wa kiasi Fulani kwenye uti wa mgongo. Lakini kama ukipinda kwa zaidi ya digrii 45, hii inachukuliwa kama tatizo.

 

 

Wakati mwingine, kibiyongo hakisababishi dalili zozote ukitoa mgongo kuonekana kupinda au kutokezea kwa nyuma. Lakini kwa baadhi ya watu huweza kusababisha dalili zifuatazo:

 • Maumivu ya mgongo na kukaza
 • Uti wa mgongo kuuma ukishikwa
 • Uchovu

Maumivu ya mgongo huweza kuwa tatizo kwa watu wazima wenye kibiyongo kwa kuwa mwili unalazimika kuweka nguvu za ziada kukabili hali hii isiyo ya kawaida

“Kama una kibiyongo kikali, dalili zaweza kuwa mbaya zaidi kadri muda unavyoenda. Waweza pia kupata shida kupumua na kula.”

Nini husababisha kibiyongo?

Katika hali hii, upindo wa asili wa sehemu ya kati ya uti wa mgongo hupinda zaidi kuliko kawaida. Kuna sababu kadhaa zinazoweza kupelekea hili:

 1. Ukaaji usiofaa – kujikunja mgongo, kuegemea kiti kwa nyuma au kubeba mizigo mizito huvuta misuli na mishipa inayoishikilia, na hivyo huongeza kupinda kwa mgongo

2. Umbile la mgongo lisilo la kawaida – kama mifupa ya uti wa mgongo haijakua inavyotakiwa, yaweza kuishia kujipanga nje ya nafasi yake stahiki

3. Matatizo katika utengenezaji wa uti wa mgongo wa mtoto kwenye tumbo la mama – hii hutokea mtoto anapozaliwa kama uti wa mgongo haukujitengeneza vizuri wakati wa ukuaji

4. Umri – kadri mtu anavyozidi kuzeeka, upindo wa uti wa mgongo huongezeka

5. Huweza pia kutokea baada ya majeraha ya mgongo kama vile ajali

Matibabu ya Kibiyongo

Kama una kibiyongo, matibabu hutegemea kiwango cha kupinda kwa mgongo, kama una dalili zinazoambatana kama vile maumivu ya mgongo, na sababu zilizopelekea kupata kibiyongo

 

Watoto wenye tatizo hili wanaweza kutibiwa na njia zisizohusisha upasuaji, ili kuzuia hali hii kuendelea kadri mtoto anavyokua. Wakati mwingine tatizo hili laweza lisihitaji tiba.

 

Tatizo la kibiyongo kwa nadra sana huhitaji upasuaji. Huhitajika tu pale ambapo hali imekuwa mbaya sana, ili kurekebisha upindo wa mgongo kuwa kawaida

 

 

Masuala ya kisaikolojia

Kwa watoto wakubwa wenye kibiyongo, wanaweza kuwa na wasiwasi au aibu kutokana na mwonekano wao au kama ikibidi wawekewe vyuma mgongoni. Masuala haya huweza kuathiri watoto kwa njia tofauti. Baadhi ya watoto huishia kujitenga na jamii na wanaweza wasipendelee kujihusisha na shughuli kama vile michezo, ambapo mwonekano wao unaweza kudhihirika.

 

Hakuna majibu ya moja kwa moja kwa masuala haya, lakini ni vyema kumsaidia mtoto kwa kumweleza kuwa hisia hizi huisha kadri muda unavyoenda

Matatizo yanayoweza kutokana na Kibiyongo

Hutokea tu kati hali ambayo ni mbaya zaidi.

 • Maumivu ya kudumu ambayo hayatulizwi na dawa
 • Matatizo ya kupumua yanayosababisha uti wa mgongo kukandamiza mapafu na njia ya hewa

 

Wakati mwingine, watu wenye kibiyongo hupata shida pale neva zinazopita kwenye uti wa mgongo zinapokandamizwa na kufinywa. Hii huweza kuingilia mawasiliano ya mishipa ya fahamu na kusababisha dalili kama vile:

 • Ganzi au kulegea kwa mikono na miguu
 • Matatizo ya usawa (balance)
 • Kushindwa kuzuia mkojo au haja kubwa

Dalili  hizi zinaashiria hatari kubwa na huchukuliwa kama dharura inayohitaji uangalizi wa haraka wa kitaalamu na upasuaji unashauriwa.

Je, naweza kujizuia nisipate kibiyongo?

 

 

Kibiyongo kinachosababishwa na ukaaji usiofaa unaweza kuzuiwa kwa kukaa vizuri na kujali mgongo wako.

Unaweza kufanya yafuatayo:

 • Usijikunje mgongo unapokaa
 • Ukae vizuri – kaa kwa kunyoosha mgongo uwe wima
 • Epuka kubeba mizigo mizito mgongoni inayovuta misuli ya mgongo
 • Fanya mazoezi mara kwa mara kuimarisha mgongo na kuufanya uwe mwepesi; mazoezi kama vile kuogelea, kukimbia, kutembea yanafaa sana kuzuia matatizo ya mgongo

Privacy Preference Center