Fahamu kuhusu Kichaa cha Mbwa na Athari zake

Utangulizi

 • Kichaa cha mbwa (Rabies), ni ugonjwa hatari wa kuambukiza unaosababishwa na virusi aina ya rabies na huweza kuwapata wanyama wote wanyonyeshao. Binadamu anaweza kuambukizwa ugonjwa huu kupitia mate ya mnyama mwenye ugonjwa huo anapong’atwa na mnyama mwenye virusi hivyo vya rabies.
 • Japokuwa watu wengi hupata ugonjwa huu kupitia mbwa kwa vile yuko karibu na binadamu, pia wanyama kama fisi, paka, popo na mbweha wanaweza kueneza ugonjwa huu. Kwakuwa virusi vinavyosababisha ugonjwa huu hukaa kwenye mate ya mnyama mwenye maambukizi, hivyo mtu aliyeambukizwa anaweza pia kumuambukiza mwingine iwapo atamng’ata au mate yake yataingia sehemu yenye jeraha.
 • Ugonjwa huu huathiri ubongo na kawaida aliyeambukizwa huugua na kufariki baada ya muda mfupi endapo hakuwahi kupata chanjo ya ugonjwa huu hapo kabla.

Nitamsaidiaje mtu aliyeng’atwa na mbwa?

Huduma ya kwanza kwa mtu aliyenga’atwa na mbwa ni kusafisha jeraha kwa maji safi yanayotiririka pamoja sabuni kwa takribani dakika 20. Baada ya kusafisha jeraha majeruhi anatakiwa kufikishwa hospitali haraka iwezekanavyo huku jeraha lake likiwa wazi bila kufunikwa na kitu chochote.

Mtu aliyeambukizwa kichaa cha mbwa huonesha dalili gani?

Muda kati ya kuambukizwa na kufikia kuonesha dalili unatofautiana kutoka mtu mmoja na mwingine kutegemeana na umbali ambao virusi husafiri kufikia ubongo. Kwa mfano mtu aliyeng’atwa shingoni atawahi kuonesha dalili kuliko aliyeng’atwa mguuni. Virusi vya rabies vikishafika kwenye ubongo wa aliyeng’atwa na mbwa huanza kuonesha dalili zifuatazo;-

 • Homa
 • Maumivu ya kichwa
 • Hofu ya maji
 • Kukasirika au kuogopa sana kwa ghafla
 • Kukosa usingizi
 • Kukosa uwezo wa kutawala mwendo wa viuongo vya mwili
 • Kuchanganyikiwa
 • Kupoteza fahamu

Dalili hizi zinapoonekana maana yake ugonjwa umeanza kushambuliaa na kuharibu ubongo na kufikia hatua hii mgonjwa hawezi kupona tena

Zifahamu dalili za mbwa mwenye kichaa

Mbwa mwenye ugonjwa huu huonesha dalili mbalimbali zikiwemo

 • kubadilika tabia yake ya awali mfano kama alikua mpole hugeuka kuwa mkali
 • kukimbiakimbia hovyo bila sababu
 • kujeruhi watu bila kuchokozwa
 • kula vitu ambavyo kwa kawaida sio chakula mfano vijiti na karatasi
 • kubweka hovyo na kubadilika sauti
 • kutoa mate mengi mdomoni kuliko kawaida

 

Namna ya kujikinga na kichaa cha mbwa

Ugonjwa huu japokuwa ni hatari sana lakini unaweza kuzuilika kwa asilimia 100 endapo wanyama watapewa chanjo dhidi ya ugonjwa huu. Pia binadamu anaweza kujikinga na ugonjwa huu kwa kupata chanjo (pre-exposure vaccine) kabla ya kung’atwa na mbwa mwenye ugonjwa huu.

8 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.