Uke wangu hauingiliki. Je, nina tatizo gani ? (Vaginismus)

Vaginismus ni tatizo la kukaza kwa misuli ya sehemu ya juu ya uke pale ambapo kitu chochote kinapojaribu kupenya au kukandamiza uke. Hali hii huweza kuambatana na maumivu yanayoweza kuwa ya kawaida au makali sana na mwanamke husika hawezi kujizuia kukaza kwa misuli hii (involuntary).

Mara chache watu huzungumzia jambo hili hivyo unaweza kuhisi kuwa peke yako lakini ni jambo linalotokea. Takwimu zinaonesha kati ya wanawake 100 duniani, hadi wanawake 17 wanasumbuliwa na tatizo hili. Pia, vaginismus inaweza kumpata mwanamke wa umri wowote, kuanzia vijana wadogo hadi walioko katika ndoa.

Chanzo na Dalili

Chanzo cha tatizo hili hakijafahamika lakini huhusianishwa zaidi na hofu ya kujamiiana kutokana na sababu za kihisia au kibaiolojia.

Sababu za kihisia ni kama:

 • Hofu kwa mfano hofu ya maumivu au kupata mimba.
 • Wasiwasi au hatia.
 • Ugomvi katika mahusiano au mwenza mkorofi.
 • Matukio kama ubakaji.

Sababu za kibaiolojia:

 • Maambukizi kama maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) au fangasi.
 • Cancer
 • Kujifungua
 • Kukoma hedhi
 • Upasuaji wa nyonga
 • Athari za madawa.

Dalili zake ni kama vile:

 • Maumivu wakati wa kujamiiana kama hisia ya kuchanika kuta za uke.
 • Mwanaume anakua kama anakutana na ukuta usiopenyeka wakati wa kujamiiana.
 • Maumivu wakati wa kufanyiwa vipimo ukeni.
 • Kukaza kwa misuli ya uke au kuacha kupumua wakati wa kuingiliwa (intercourse)

Tatizo hili linaweza kutibika kwa njia ya kujizoesha kwa namna mbili. Kwanza, kwa kufanya mazoezi ya Kegeli (Kegel Exercises) ambapo mhusika hukaza na kulegeza misuli inayohusika kuzuia mkojo ili kujijengea maamuzi juu misuli hii. Unaweza kujifunza zaidi kuhusu mazoezi ya Kegeli hapa.

Pili, kwa msaada wa daktari au mtaalamu wa mambo ya wanawake, vifaa maalumu vya ukubwa mbalimbali (Vaginal Dilators) huingizwa ukeni ili kuuzoesha uke na kuondoa hali ya woga. Zoezi hili linaweza kufanywa na mhusika mwenyewe au kwa msaada wa mwenza wake kwani ni swala la kujizoesha.

Kadhalika, daktari wa ushauri nasaha anaweza kusaidia kuondoa mawazo hasi na hofu kuhusu kujamiiana na kusaidia kuondoa tatizo hili iwapo chanzo chake ni cha kisaikolojia. Pamoja na hayo, ni muhimu kujua chanzo cha tatizo kabla ya kutibu na kuna mambo mengi sana yanayoweza kusababisha maumivu wakati wa kujamiiana hivyo ni muhimu kumuona daktari kwa msaada zaidi.

2 thoughts on “Uke wangu hauingiliki. Je, nina tatizo gani ? (Vaginismus)

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Privacy Preference Center