DALILI ZA AWALI ZA UGONJWA WA UKIMWI

DALILI ZA AWALI ZA UGONJWA WA UKIMWI

DALILI ZA AWALI

Dalili za ugonjwa wa UKIMWI huanza kuonekana kuanzia siku 7 hasi siku 21 baada ya maambukizi kutokea iwapo mgonjwa hayupo katika matumizi ya dawa za kufubaza virusi hivyo

Asilimia arobaini (40%) mpaka (90%) ya wagonjwa walioambukizwa virusi vya UKIMWI huanza kupata dalili za awali kati ya wiki moja hadi tatu tangu kuambukizwa. Katika kipindi hichi, virusi hivi vipya vinakua katika mapambano makali na kinga ya mwili na hupelekea kuonekana kwa dalili zifuatazo.

 

HOMA

Huku ni kuongezeka kwa joto la mwili juu ya halijoto ya kawaida ya mwili. Mtu hujisikia baridi kali japokuwa mwili wake ni wa moto na huweza kuambatana na kutetemeka.

KUVIMBA KWA TEZI(MITOKI)

Tezi limfu hizi huwa katika makundi ambayo hunapatikana shingoni, chini ya kidevu, kwapani na kwenye nyonga. Katika hali ya kawaida, tezi hizi hazipaswi kuhisiwa zikipapaswa lakini baada ya maambukizi huongezeka ukubwa hadi kufikia ukubwa wa punje la harage. Pia huambatana na maumivu zikishikwa ama bila kushikwa.

UPELE

Asilimia ishirini (20%) mpaka hamsini (50%) ya wagonjwa hupata vipele hasa maeneo ya kiwiliwili.Vipele hivi huwa vidogo, huweza kujaa maji na kuacha vidonda pale vikipasuka. Huweza kuambatana na muwasho  na kubadilika kwa rangi ya Ngozi ya sehemu iliyoathirika kuwa nyekundu au nyeusi zaidi.

 

DALILI NYINGINEZO

Hizi ni pamoja na maumivu ya kichwa na koo, vidonda vya kinywa na sehemu za siri. Baadhi ya watu huweza kuhisi kichefuchefu, kutapika na kuharisha. Wengine pia huishiwa nguvu na huweza kupata ganzi mikononi na miguuni.

Dalili hudumu kwa muda wa wiki moja hadi mbili na hufuatiwa na kipindi cha VVU bila dalili. Kipindi hichi kinaweza kudumu kwa miaka mitatu (3) hadi ishirini (20) na zaidi. Mwishoni mwa kipindi hiki huwa na dalili mbali mbali ambazo zimeelezewa katika makala inayofuata (Sehemu ya pili).


Leave a comment