DALILI ZA UGONJWA WA UKIMWI (SEHEMU YA PILI)

DALILI ZA UGONJWA WA UKIMWI (SEHEMU YA PILI)

DALILI ZA UGONJWA WA UKIMWI

Hali ya mgonjwa kutotumia dawa za ARV hupelekea virusi kuongezeka kwa kasi kubwa na kuendelea kudhoofisha kinga ya mwili na hatimaye kinga hushindwa kudhibiti virusi hivi. Dalili za mwanzo kama homa, upele na kuvimba kwa tezi hujirudia. Fangasi za kinywani na kooni, kukohoa, kupungua uzito na magonjwa ya ngozi hutokea pia katika hatua hii.

Kushuka kwa kinga ya mwili hukaribisha magonjwa nyemelezi yaweze kuushambulia mwili. Magonjwa nyemelezi yanaweza kusababishwa na bakteria, virusi na vimelea ambavyo kwa kawaida hudhibitiwa. Magonjwa hayo pamoja ni haya yafuatayo:

 

KIFUA KIKUU

Hatari ya kupata kifua kikuu kwa waathirika wa VVU huongezeka kwa asilimia 20 mpaka 30. Huu ni ugonjwa unaoweza kuathiri mapafu au sehemu nyingine za mwili. Kwa wagonjwa wa UKIMWI dalili hujitokeza endapo kiwango cha CD4 kiko chini ya 500. Mgonjwa huonesha dalili zifuatazo;

 • Maumivu ya kifua na kikohozi cha muda mrefu, wakati mwingine mgonjwa anaweza kukohoa damu kwa kiasi kidogo.
 • Homa kali inayoambatana na kutoka jasho jingi wakati wa usiku.
 • Kupungua kwa uzito wa mwili kwa kiasi kikubwa.
 • Kuvimba kwa tezi (Mitoki)
 • Kupumua kwa shida
 • Maumivu ya viungo na kupooza kwa viungo vya mwili endapo ugonjwa umeathiri uti wa mgongo.
 • Kuishiwa nguvu na matatizo ya mijongeo iwapo ugonjwa umeathiri mfumo wa fahamu.

SARATANI

Waathirika wa VVU wapo katika hatari kubwa zaidi ya kupata saratani mbali mbali zinazosababishwa na virusi. Saratani hizo ni;

SARATANI YA KAPOSI

Saratani hii huathiri chembe hai za ukuta wa ndani wa mishipa ya damu. Mgonjwa huwa na alama za mabaka mekundu au zambarau juu ya ngozi. Mabaka haya hukua na kutengeneza vinundu,na hii huweza kuonekana  kwenye ngozi laini ya midomo.

SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI

Waathirika wa virusi vya UKIMWI wako katika hatari mara sita zaidi ya kupata kansa ya shingo ya kizazi ukilinganisha na wasio na maambukizi. Ugonjwa huu husababishwa na virusi aina ya HPV ambao baada ya muda hubadilisha seli za mlango wa uzazi na mabadiliko hayo huenda yakapelekea mtu kupata saratani.

Dalili za saratani ya shingo ya kizazi ni zifuatazo;

 • Kutokwa damu ukeni kusiko kawaida mfululizo.
 • Kupata maumivu makali ya tumbo na nyonga.
 • Maumivu wakati wat tendo la ndoa.
 • Kutokwa na majimaji yenye harufu ukeni kusiko kawaida.

Muda unavyosonga zaidi, ugonjwa huu unaweza kusambaa kwenda tumboni, mapafuni au popote pale mwilini na mgonjwa atapata dalili kutokana na sehemu iliyoathiriwa.

 

Saratani nyingine ni kama vile limfoma ambayo imesababisha vifo vya karibu asilimia kumi na sita (16%) ya watu wanaoishi na UKIMWI na husababishwa na virusi vya Hepesi kwa mfano limfoma ya Burkitt. Pia wagonjwa wa UKIMWI huweza kupata saratani ya koo, saratani ya ngozi na saratani nyingine zinazoweza kutokea sehemu mbali mbali za mwili.


Leave a comment