KUJIFUNGUA KABLA YA MUDA ULIOTEGEMEWA (PREMATURE BIRTH) HUSABABISHWA NA NINI?

KUJIFUNGUA KABLA YA MUDA ULIOTEGEMEWA (PREMATURE BIRTH) HUSABABISHWA NA NINI?

Kila mwaka takribani watoto milioni 15 duniani huzaliwa kabla ya miezi 9 kutimia na idadi inazidi kuongezeka-WHO

Kujifungua kabla ya wakati uliotegemewa yaani kabla ya tarehe mama mjamzito aliyoambiwa hospitali ni hali ambayo hutokea mama mjamzito hujifungua katika kipindi baada ya wiki 20 (miezi 5) lakini kabla ya wiki 37 (miezi 9) ya ujauzito.

Mtoto kuzaliwa kabla ya wakati anaweza kupata madhara ya kiafya kama vile kuzaliwa akiwa na uzito mdogo, kuzaliwa akiwa na matatizo ya upumuaji, kuzaliwa akiwa na matatizo ya kuona, kuzaliwa akiwa na ogani na viungo vya mwili ambavyo havijakua vizuri pia huwa huwa hatarini kupata tatizo la kupoteza joto (hypothermia).

 

Vihatarishi na visababishi vya tatizo la kujifungua mapema

Tatizo hili huweza kutokea kwa ujauzito wowote ule lakini kuna sababu ambazo zimekuwa zikihusishwa zaidi kuongeza hatari ya kujifungua mapema sababu hizo ni pamoja na;

 • Matumizi ya pombe, na uvutaji wa sigara wakati wa ujauzito.
 • Kuwa na magonjwa sugu ya kiafya kama vile kisukari na matatizo ya presha.
 • Msongo wa mawazo kupita kiasi wakati wa ujauzito.
 • Kuwa na tatizo la kiafya katika mfumo wa uzazi kama vile mji wa mimba (uterus), mirija ya mayai au shingo ya kizazi.
 • Kupata maambukizi hasa katika maji maji yanayokuwa katika mji wa mimba wakati wa ujauzito (amniotic fluid).
 • Mtoto kuwa na matatizo ya kimaumbile.
 • Pia kuwa na historia ya kuwahi kujifungua kabla ya wakati.
 • Kuwa na ujauzito wa mapacha.

 

Dalili za tatizo la kujifungua kabla ya wakati.

Uonapo dalili hizi wakati wa ujauzito ni vyema kuwahi kumwona daktari kwani huweza kuwa ni dalili za mwanzo za tatizo la kujifungua kabla ya wakati.

 • Kutoka damu au matone ya damu ukeni wakati wa ujauzito.
 • Misuli ya eneo la tumbo hasa chini ya kitovu kusinyaa mara kwa mara.
 • Kuhisi mara kwa mara kama kukaza kwa misuli ya tumbo.

 

Nifanye nini kupunguza hatari ya kupata tatizo kujifungua mapema.

 • Hudhuria mara kwa mara kliniki na mweleze daktari wako kila dalili unayoihisi isiyo ya kawaida wakati wa ujauzito, hii itamsaidia daktari kufuatilia afya yako na ya mtoto wakati wa ujauzito.
 • Kula chakula bora wakati wote wa ujauzito pia epuka kula vyakula vyenye mafuta kwa wingi.
 • Epuka matumizi ya vilevi, uvutaji wa sigara au kukaa maeneo ambayo wavutaji wa sigara hupendelea kukaa.

Leave a comment