Kujikojolea kwa watoto; Jua sababu zake na matibabu

Kujikojolea kwa watoto; Jua sababu zake na matibabu

Utangulizi

 • Enuresis kama inavyojulikana kwa kitaalamu ni tatizo la kukojoa bila ufahamu wako (kujikojolea) licha ya kwamba umefikia umri wa kuweza kuzuia hali hiyo kutokea
 • Kwa kawaida watoto chini ya miaka mitano misuli yao ya kibofu haijakuwa na kukomaa vya kutosha kuweza kuzuia mkojo mwingi hasa wakati wa usiku na ni kawaida kwao kukojoa angali wamelala (Physiological enuresis)
 • Shida inakuja pale mtoto amevuka miaka mitano,hana tatizo lolote la kianatomiki linalojulikana kuzuia mtoto asibane mkojo na bado anajikojolea wakati amelala usiku
 • Sawa mtoto anaweza pata ajali (kujikojolea) hata mara mbili kwa mwaka lakini Enuresis hutokea pale mtoto atajikojolea mara mbili kwa wiki kwa miezi mitatu mfululizo. Hivyo basi anastahili kupata kumwona daktari kufanyiwa uchunguzi zaidi
 • Watoto wengine pia huweza kujikojolea wakiwa macho mchana au wengine kufanya hivyo mchana na usiku

Aina zake

 • Kuna aina ya kwanza ambapo mtoto hajawahi maishani mwake kuweza kubana mkojo tangia azaliwe yaani mtoto amevuka miaka mitano na bado anajikojolea
 • Na aina ya Pili,ni kwa watoto walioweza kujizuia kujikojolea baada ya kuvuka miaka mitano kwa muda wa mpaka miezi sita ila baada ya hapo wakashindwa na kuanza kujikojolea tena

Dalili zake

 • Kuongezeka kwa hamu na mara za kwenda kukojoa
 • Kutokwa na mkojo pale mtoto mfano.anapokohoa au anapotekenywa
 • Kukojoa bila kujitambua wakati wa usiku akiwa amelala

Visababishi vyake

 1. Kuna baadhi ya vinasaba vinaaminika kuchangia kupitishwa kwa vizazi vijavyo
 2. Kuchelewa kukua kwa maumbile ya mtoto mfano mtoto akawa na kibofu kidogo kulinganisha na umri wake
 3. Kuongezeka kwa utengenezaji wa mkojo wakati wa usiku kuliko kawaida kutokana na utengenezwaji mdogo wa homoni iitwayo Anti Diuretic (ADH) wakati wa usiku
 4. Woga ambapo mtoto anaweza upata labda kwa kupigwa na wazazi n.k
 5. Kubana mkojo kwa watoto na kulala wakiwa na kibofu kilichojaa sana

Nini cha kufanya

 1. Kwanza ni kubadili mambo mbalimbali kama mlo wa mtoto hasa wa usiku kabla ya kulala kwa kupunguza vimiminika anavyotumia,pia mtoto aende uwani kabla ya kulala
 2. Kama bado anaendelea na dalili,ni muhimu kwenda hospitali iliyo karibu yako kujua kama mwanao ana tatizo lolote la kitabibu inayozuia mtoto ashindwe kubana mkojo na kupewa matibabu kama dawa za kupunguza utengenezwaji wa mkojo hasa wakati wa usiku
 3. Huweza kuanza mazoezi maalum ya kufundisha kibofu chake kiweze kujua muda wa kukojoa na muda wa kubana mkojo (Bladder Training)
 4. Bladder training inaweza kuelekezwa na madaktari husika namna ya kumsaidia mtoto hata akiwa nyumbani aweze kukojoa kwa hiari yake hata wakati amelala
 5. Zawadi.baadhi ya watoto wameonekana wakipata nafuu kwa kuahidiwa zawadi kwa kila usiku atakaomaliza bila kujikojolea mfano,kumpa pipi au kumpikia chakula akipendacho n.k mpaka itakapokuwa tabia kulala bila kujikojolea
 6. Kwa nchi zilizoendelea wana pampasi zinazoweza kutambua unyevu unyevu na kupiga muito wa kumuamsha mtoto wakati anaanza kujikojolea (Bed wetting Alarms)

Leave a comment