Kwanini nahisi maumivu wakati wa kujamiiana ? (dyspareunia)

Kwanini nahisi maumivu wakati wa kujamiiana ? (dyspareunia)

Tendo la kujamiiana linapaswa kuwa tendo la kuvutia na bila shaka utajiuliza maswali mengi iwapo maumivu yataambatana na tendo hilo. Zifuatazo ni sababu zinazoweza kusababisha maumivu wakati wa tendo la ndoa:

1. Vaginismus

Hili ni neno la kitaalamu linalomaanisha kukaza kwa misuli ya uke kusiko kwa hiari wakati wa tendo la ndoa. Hii hutokea pale ambapo mwanamke anakua na hofu ya kuumizwa wakati wa kuingiliwa.

 

2. Maambukizi katika uke

Hii hutokea mara kwa mara pale ambapo uke unashambuliwa na vijidudu kama vile fangasi. Hatimaye sehemu iliyo na maambukizi huweza kuwa na maumivu wakati wa kujamiiana.

 

3. Uvimbe katika mji wa mimba

Iwapo kuna uvimbe katika mji wa mimba (Uterus) kama vile uvimbe unaofahamika kitaalamu kama fibroids, huweza kusababisha maumivu wakati wa kujamiiana hasa pale mwanamke anapoingiliwa kwa nguvu (deep penentration).

 

4. Ukavu katika uke

Hii hutokea iwapo mwanamke hajaandaliwa vizuri kabla ya kuingiliwa hivyo hukosa msisimko wa kutosha kuzalisha majimaji yanayolainisha uke. Pia huweza kusababishwa na hofu wakati wa kujamiiana hali inayopelekea mwanamke kutoshiriki kikamilifu na kukosa msisimko. Hali ya kukoma kwa hedhi pia husababisha ukavu ukeni kutokana na kukosekana kwa homoni mbalimbali. Yote haya huweza kusababisha maumivu wakati wa kujamiiana.

 

5. Majeraha

Mwanamke anaweza kuhisi maumivu wakati wa kujamiiana iwapo bado hajapona majeraha yatokanayo na kujifungua, upasuaji au ubakaji.

Maumivu wakati wa kujamiiana huweza kutibiwa kutegemea chanzo cha tatizo. Mwanamke anapaswa kusubiri walau wiki sita baada ya kujifungua kabla ya kujamiiana tena. Iwapo shida ni ukavu ukeni, ni vema kutumia vilainishi visivyo na kemikali (water-based lubricants). Iwapo ukavu unasababishwa na ukomo wa hedhi, ni vema kuwasiliana na daktari akuandikie dawa za estrojeni au madawa mengine.

Ni vizuri pia kuondoa mawazo ya kujilaumu (guilt) au hisia za matukio mabaya ya nyuma kama ubakaji. Maumivu yakiambatana na dalili kama kutoka damu, hedhi zisizoeleweka, ute usio wa kawaida au kukaza misuli ya uke kusiko kwa hiari ni vema kumtembelea daktari kwa msaada zaidi.


Leave a comment