MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UKIMWI

MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UKIMWI

Virusi vya Ukimwi huambukizwa (VVU) kwa njia ya ngono Isiyo salama na mwenza aliyeathirika, kuongezewa damu au mazao ya damu yenye maambukizi ya VVU na maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Virusi vya Ukimwi hupatikana kwenye damu na majimaji ya mwili kama shahawa, majimaji ya ukeni na njia ya haja kubwa na maziwa ya mama, kwa nadra sana VVU huweza kupatikana kwenye mate, makohozi, machozi, jasho, kamasi, mkojo au matapishi. Ili kusababisha maambukizi ya VVU ni lazima viingie katika mzunguko wa damu ya mtu asiye na maambukizi kupitia mipasuko au vidonda vilivyopo kwenye ngozi,ukeni, uume, njia ya haja kubwa au mdomoni au kwa kupitia kujichoma na vifaa vyenye ncha kali vilivyo tumika na mtu mwenye maambukizi.

 

KUONGEZEWA DAMU ISIYO SALAMA

  • Usambazaji wa VVU kwa kupitia damu unaweza kuwa kwa kuongezewa damu au mazao ya damu ambayo haijafanyiwa uchunguzi wa magonjwa ambukizi kama VVU. Tafiti zinaonesha takribani asilimia 2% mpaka 4% ya virusi vya ukimwi huchangiwa kwa kuongezewa damu yenye maambukizi. Mbu au wadudu wengine wang’atao pia hawawezi kuambukiza na kusambaza VVU.

Pia virusi vya Ukimwi huambukizwa kwa kuchangia vifaa vyenye ncha kali ambavyo havijasafishwa njia za kitaalamu kama sindano, viwembe, mashine za kunyolea na vifaa tiba mbalimbali vinavyotumika kwa wagonjwa wakati wa matibabu, watu wanaochanja chale, uchoraji wa chata mwilini na kutahiri. Hii huchangia kwa asilimia 0.23% ya jumla ya maambukizi yote. Pia VVU inaweza kuambukizwa kwa kuchangia sindano, hii hutokea zaidi kati ya watumiaji wa madawa ya kulevya kwa njia ya sindano.

Zaidi wahudumu wa afya wanaweza kupata maambukizi kwa kujichoma na sindano iliyotumika kwa mtu mwenye maambukizi.

NGONO ISIYO SALAMA

Zaidi ya asilimia 90% ya watu wazima wanaoishi kusini mwa Jangwa la Sahara hupata maambukizi ya VVU kupitia ngono isiyo salama kutoka kwa wenza wenye maambukizi ya VVU. Hatari ni kubwa zaidi kwa ngono ya ukeni na ulawiti, ngono ya mdomoni huleta maambukizi ikiwa kuna mipasuko mdomoni. Vitendo vinginevyo vya ngono ambavyo havihusishi mabadilishano ya viowevu vya mwili kama vile kugusana, kukumbatiana, kushikana mikono haiwezi kusababisha maambukizi ya VVU.

  • Kufanya ngono isiyo salama kumepelekea visa vingi zaidi vya maambukizi ya VVU kote ulimwenguni, huku mwingiliano baina ya watu wa jinsia tofauti ukichangia visa zaidi. Makadirio ya hatari ya kusambazwa kwa VVU kwa kila kitendo cha ngono baina ya watu wa jinsia moja, yanaonekana kuwa zaidi kwa mara 10.

Uwezekano wa  kuambukizwa kutokana na ulawiti uko juu sana na ingawa hatari ya kuambukizwa kupitia ngono ya mdomoni iko chini, lakini uwezekano huo bado upo. Hatari ya kuambukizwa huongezeka zaidi kama una magonjwa mengine ya zinaa, kama vile kisonono, klamidia na vidonda sehemu za siri kwa mara tano zaidi.

Wingi wa virusi kwa mtu aliyeambukizwa huongeza hatari mara dufu katika umbukizwaji wa VVU kwa njia ya ngono na pia kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

MAAMBUKIZI KUTOKA KWA MAMA KWENDA MTOTO

  • VVU vinaweza kusambazwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito, kujifungua au kunyonyesha. Njia hii ni ya tatu kwa kuchangia katika kusambaza VVU kote duniani. Bila matibabu, hatari ya maambukizi ya VVU wakati au baada ya kuzaliwa ni takribani 15% mpaka 45%.
  • Vichochezi mbalimbali kama kuchelewa kugundulika kwa hali ya vvu ya mama mjamzito, kiwango kikubwa cha VVU katika damu ya mama mjamzito, kutotumia au kutozingatia matumizi sahihi ya dawa za kupunguza makali ya VVU na kufanya ngono isiyo salama kipindi cha ujauzito humweka mtoto katika hatari kubwa ya kupata maambukizi.
  • Hatari ya kusambaza VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto inaweza kupunguzwa hadi 5% kwa kutumia matibabu na njia sahihi zilizo elekezwa kliniki wakati na baada ya ujauzito.

Leave a comment