MATIBABU YA UGONJWA WA UKIMWI

MATIBABU YA UGONJWA WA UKIMWI

MATIBABU YA UKIMWI

Mpaka sasa ugonjwa wa UKIMWI hauna tiba. Lakini hii haimaanishi kupata maambukizi ya virusi vya UKIMWI ni mwisho wa maisha, kwa sababu kuna dawa nyingi ambazo zinatumika kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI.

Dawa hizi huitwa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI (ARVs). Mtu yeyote anapaswa kuanza kutumia dawa hizi za ARV punde tu baada ya kugundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

Dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI mara nyingi ni muunganiko wa dawa tatu kutoka makundi tofauti ya dawa. Lengo kuu la dawa hizi ni kupunguza kiwango cha virusi vya UKIMWI mwilini. Mara nyingi dawa hizi tatu zimetengenezwa na kuwa kidonge kimoja au viwili ambazo mgonjwa hunywa kila siku.

Kwa sababu dawa hizi za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI ni muunganiko wa dawa zaidi ya moja, hii husaidia dawa hizi kuwa na uwezo mkubwa wa kupunguza idadi ya virusi vya ukimwi kwenye damu pia huzuia kujengeka kwa usugu wa madawa ambao hufanya matibabu ya ugonjwa wa UKIMWI kuwa magumu zaidi.

Kwa Tanzania dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI zina muunganiko wa dawa tatu tenofoviri, lamivudine na doltegravir, lakini kuna miunganiko mingine ya dawa hizi amabzo hutumika kulingana na hali ya mgonjwa binafsi na ushauri wa daktari. Hivyo mgonjwa anashauriwa kufuata maelekezo ya daktari wake.

 

KUANZA NA KUENDELEA NA UTUMIAJI WA ARTs

  • Muongozo wa matibabu ya UKIMWI wa Tanzania unaagiza wagonjwa wote kuanza kutumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI, mara tu baada ya kugundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
  • Kabla ya kuanza kutumia dawa daktari huchukua vipimo vya kuangalia kiwango cha virusi kwenye damu, daktari hurudia kipimo hiki baada ya miezi sita ili kuangalia kama virusi vinapungua katika damu baada ya kuanza kutumia dawa.
  • Kipimo hiki huendelea kupimwa mara moja kwa mwaka endapo virusi vitaonekana kutokupungua kwenye damu. Kama idadi  ya virusi vya UKIMWI hakitashuka basi daktari huangalia uwezekano wa kubadilisha muunganiko wa dawa.

Kwa matokeo mazuri mgonjwa anapaswa kuendelea na matumizi sahihi ya dawa kama ambavyo daktari ameelekeza.

Matumizi sahihi ya dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI huuwezesha mwili kuwa na kiwango cha chini sana cha virusi hivyo kinga hubaki imara na kusaidia kutopata magonjwa nyemelezi na pia hupunguza hatari ya kusambaza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa watu wengine.

 

Wasiliana na daktari wako iwapo utakumbana na matatizo yeyote ya kiafya kutokana na kutumia dawa.


Leave a comment