Nina harufu mbaya ya kwapa, je nifanye nini?

Nina harufu mbaya ya kwapa, je nifanye nini?

Jasho ni moja ya njia maalumu ya mwili ya kurekebisha kiwango cha joto la mwili, ila inapofika wakati jasho hili linaanza kutoa harufu mbaya huwa kero kwa mtu anayetoa harufu na kwa jamii nzima inayomzunguka.

Kwa kawaida jasho huwa halina harufu, kwani jasho ni mchanganyiko wa maji na aina mbalimbali za madini ya chumvichumvi yanayotolewa kama taka mwili,

Harufu mbaya ya kwapa husababishwa na bakteria ambao humeng`enya aina fulani ya protini inayozalishwa pamoja na jasho kutoka katoka tezi maalumu za jasho ziitwazo apocrine glands. Tezi hizi zinapatikana katika maeneo ya matiti, maeneo ya sehemu za siri, katika kope za macho huku idadi kubwa ya tezi hizi ikiwa katika makwapa hivyo kupelekea kiwango kikubwa cha jasho kuzalishwa katika maeneo ya makwapa.

Jasho hasa la kwapa kutoa harufu ni jambo la kawaida lakini kwa baadhi ya watu hali hii ya kunuka kwapa huwa sugu sana na hivyo kuwa kero kwao na jamii kwa ujumla.

Ili kupunguza harufu au kuimaliza kabisa yapaswa kupunguza pia kiwango cha jasho unalozalisha kwa siku kwa kufanya yafuatayo;

  • Kula mlo kamili na fanya mazoezi ili kupunguza mwili, kwa sababu watu wanene huathiriwa sana na tatizo hili kwa sababu ya mikunjo mikunjo ya ngozi yao hivyo kutoruhusu jasho kukauka mwilini.
  • Vaa nguo za pamba , nguo za aina hii husharabu (hunyonya) jasho la mwili na kukuacha mkavu, epuka pia nguo zinazokubana sana.

  • Tumia manukato mbalimbali ili kupambana na harufu pia tumia dawa maalumu zinazoweza kupunguza kiwango cha jasho linalizalishwa kwenye makwapa (muone daktari wako kwa kupata dawa hizi)

  • Kuwa na tabia ya kuoga mara kwa mara ili kuondoa kiwango cha jasho kinachokuwa kimezalishwa hivyo kutoruhusu bakteria kufanya mmeng’enyo. Pia kila baada ya kufanya shughuli yoyote ya kukutoa jasho, ni vizuri kutumia medicated soap ili kuua bakteria wanaozalisha harufu mbaya.

  • Epuka vyakula na vinywaji vinavyosababisha uzalishaji mkubwa wa jasho. Mfano vyakula kama pilipili, kahawa, pombe, vitunguu.

  • Nyoa nywele za kwapani na tunza makwapa yako katika hali ya usafi. Kwa sababu uwepo wa nywele hizi husababisha jasho kutokauka. hivyo bakteria kuzalisha harufu kutokana na jasho hili.

  • Badilisha nguo na kuvaa nguo safi kila siku ili kupunguza mrundikano wa jasho.

Muone daktari wako endapo una matatizo yafuatayo.

1.Ikiwa unatoka jasho kwa wingi sana wakati wa usiku mpaka unalowanisha nguo au shuka zako.

2. Unatokwa na jasho kwa wingi kuliko kawaida ulivyozoea

3. Unatoka jasho kipindi cha baridi.

4. Jasho lina kunyima uhuru wa kufanya kazi zako za kila siku.

Uzalishaji wa jasho usio wa kawaida unaweza kuwa ishara ya uwepo wa tatizo la kiafya hivyo ni vyema kumuona daktari wako haraka iwezekanavyo.


Leave a comment