Unatamani kufahamu njia za uzazi wa mpango kwa wanaume

Unatamani kufahamu njia za uzazi wa mpango kwa wanaume

Swala la uzazi wa mpango lianonekana kuwa wajibu wa mwanamke lakini hata wanaume wana njia za uzazi wa mpango. Ingawa sio nyingi kama kwa wanawake, wanaume wanaweza kujihusisha na uzazi wa mpango kwa kutumia njia zifuatazo:

 

1. Kondomu za kiume:

Hii ndio njia iliyozoeleka na yenye uhakika zaidi wa kuweza kuzuia mimba. Pia inafaida ya kumkinga mtumiaji dhidi ya magonjwa ya zinaa. Hufanya kazi kwa kuzuia mbegu za kiume zisifike kwenye uke hivyo urutubishaji hautokei.

Kondomu zinaweza kuzuia mimba kwa uhakika wa asilimia 98 iwapo zikitumika vizuri. Matumizi yasiyo sahihi hushusha utendaji kazi hadi asilimia 82. Tatizo hutokea iwapo mtumiaji hajui jinsi ya kuvaa na kuitumia. Matumizi mabaya ya kondomu huweza kupelekea kondomu kuteleza na kutoka au kupasuka wakati wa kujamiiana.

Kwanza, kondomu hutumika mara moja tu. Pia kumbuka kuvaa kondomu kabla kabisa ya kujamiiana. Hii ni kwasababu wakati wa kujamiiana mbegu hutoka kwa kiwango kidogo kabla ya kufika kileleni hivyo huweza kupunguza utendaji kazi wa kondomu kama isipovaliwa kabla ya tendo kuanza.

  • Fungua pakiti kwa kuchana pembezoni kabisa kwa umakini ili usichane kondomu iliyopo ndani.
  • Vaa kondomu katika uume uliosimama kwa kubonyeza sehemu ya mbele ya kondomu ili kuondoa upepo. Angalia usitoboe kwa kucha. Hii huacha nafasi ya shahawa pindi utakapofika kileleni. Usipoondoa hewa, shahawa zitakapotoka hugandamizana na hewa iliyomo ndani na huweza kupasua kondomu.
  • Ukiwa bado umebonyeza sehemu ya mbele, valisha ringi kwenye kichwa cha uume na kisha viringisha taratibu kuelekea kwenye shina la uume hadi mwisho.
  • Usivae kondomu zaidi ya moja wala usitumie vilainshi vya mafuta kwani huweza kupelekea kupasuka.
  • Baada ya kutumia, vua kondomu kwa kuviringisha ringi kuelekea kwenye kichwa cha uume kabla haujasinyaa.
  • Tupa kondomu iliyotumika kwenye pipa la taka au choo cha shimo lakini sio choo cha kukalia.

2. Ufungaji wa mirija ya korodani (Vasectomy)

Huu ni upasuaji wa kawaida usiohitaji kulazwa ambapo njia ya mbegu za kiume hukatwa na kufungwa kabla ya kufikia shahawa. Njia hii ni ya kudumu na inauhakika wa asilimia 99 katika kuzuia mimba. Baada ya upasuaji, mwanaume anaweza kufanya mapenzi kama kawaida na akifika kileleni, shahawa hutoka kama kawaida lakini hazitakua na mbegu hivyo haziwezi kusababisha mimba.

3. Kumwaga shahawa nje ya uke

Hii ni moja ya njia kongwe kabisa na huweza kuzuia mimba kwa uhakika wa asilimia 75 tu. Huhusisha kutoa uume punde tu unapohisi kufika kileleni ili shahawa zimwagike nje ya uke. Ni njia isiyo ya kuaminika sana kwani shahawa huweza kupenyeza na kutoka kidogo wakati wa kujamiiana. Pia huihataji dhamira ya hali ya juu na huleta usumbufu wakati wa kujamiiana. Pamoja na hayo ni bora kuliko kutokutumia kabisa na huwa bora zaidi ikitumiwa sambamba na njia nyingine za kuzuia mimba.


Leave a comment