UTANGULIZI WA UGONJWA WA UKIMWI

UTANGULIZI WA UGONJWA WA UKIMWI

Upungufu wa kinga mwilini (UKIMWI) 

Ni ugonjwa unaoasababishwa na VVU (yaani Virusi Vya UKIMWI). Ugonjwa huu hupunguza uwezo wa mwili kupambana na magonjwa nyemelezi. Virusi hawa hushambulia seli za mfumo wa kinga ya mwili ambazo huzuia mwili usivamiwe na wadudu mbalimbali wanaosababisha magonjwa, hivyo kudhoofisha uwezo wa mwili kupambana na magonjwa nyemelezi kama vile neumonia(pneumonia) na kifua kikuu (TB).

Chimbuko la Virusi vya Ukimwi (VVU) linaaminika kuanza katika Bara la Afrika, Katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa mnamo mwaka 1920 ambapo virusi hawa walihama kutoka kwa Wanyama jamii ya Sokwe kwenda kwa binadamu. Zaidi ya nusu karne baadae ndipo jamii ya wanasayansi wa afya walipogundua maambukizi ya ugonjwa huo mpya wa UKIMWI.

 

TAKWIMU ZA UGONJWA WA UKIMWI

UKIMWI ni miongoni mwa magonjwa hatari katika karne ya 21. Inakadiriwa mpaka kufikia 2020 idadi ya watu milioni 37.6 wameambukizwa na katika hawa, milioni 35.9 ni watu wazima na milioni 1.7 ni watoto chini ya miaka 15. Watu milioni 1.5 wamepata maambukizi ya VVU ndani ya mwaka 2020, hii inaashiria kupungua kwa kasi ya maambukizi mapya kwa asilimia 30 tangu mwaka 2010, na kati ya haya maambukizi mapya, watu wazima walikua milioni 1.3 na watu 160,000 walikua ni watoto chini ya miaka 15. Zaidi ya watu milioni 34.7 mpaka sasa wamepoteza maisha kwa ugonjwa wa UKIMWI. 

AFRIKA MASHARIKI

 

  • Afrika ya mashariki na kusini ni eneo lililoathirika zaidi na maambukizi ya VVU na ina wakazi wa asilimia 6.2 ya watu wanaoishi duniani, lakini ina watu zaidi ya nusu (54%) ya wanaoishi na VVU duniani milioni 20.6 kwa takwimu za mwaka 2018, kulikiwa na maambukizi 800,000, karibu na nusu ya maambukizi yaliyotokea duniani.

TANZANIA

  • Nchini Tanzania mwaka 2017 kulikua na maambukizi mapya milioni 1.4, ngono zembe ikiwa inaongoza kama njia ya maambukizi ya VVU kwa asilimia 80% nchini Tanzania. Maambukizi ya VVU ni makubwa kwa makundi ya watu wanaotumia dawa za kulevya (16-51%), wanaume wanaofanya mapenzi ya Jinsia moja (22-42%), watu wanaofanya biashara ya ngono, na wanaoendesha magari ya kwenda nchi na nchi (14-35%). Wanawake inaonekana wanapata maambukizi zaidi (6.3%) kuliko wanaume (3.9%) kutokana na takwimu.

 

Mashirika ya kupambana na UKIMWI kama UNAIDS na mashirika ya kimataifa yameweka malengo ya kuondoa maambukizi mapya ya VVU kufikia mwaka 2030. Serikali ya Tanzania inaunga mkono juhudi hizo kwa kuimarisha utoaji wa huduma za afya na matibabu kwa wagonjwa wa UKIMWI. Hii imepelekea kupungua kwa maambukizi mapya ya VVU ukilinganisha na miaka ya nyuma.


Leave a comment