UZINGATIAJI WA DAWA ZA KUFUBAZA VIRUSI VYA UKIMWI

UZINGATIAJI WA DAWA ZA KUFUBAZA VIRUSI VYA UKIMWI

UZINGATIAJI WA DAWA ZA KUFUBAZA VIRUSI VYA UKIMWI

Uzingatiaji wa dawa za kufubaza virusi vya ukimwi ni pamoja na kutumia dawa sahihi,kiwango sahihi na kwa muda sahihi kama ilivyoshauriwa na mtoa huduma wa afya.

Ushauri kuhusu uzingatiaji wa dawa za kufubaza virusi vya ukimwi ni njia mojawapo ya kupunguza kuenea kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi na ushauri huu inabidi ufanyike kabla mgonjwa hajaanza kutumia dawa za kufubaza virusi vya ukimwi(ART) na liwe ni zoezi endelevu kwa sababu dawa hizi inabidi zitumike kwa Maisha.

Ni muhimu kwa mtoa huduma za afya kuandaa mazingira rahisi na wezeshi ili kumrahisishia mgonjwa kukubali na kutambua madhara ya kutokuzingatia matumizi sahihi ya dawa za kufubaza virusi vya ukimwi

 

MADHARA YA KUTOKUZINGATIA MATUMIZI SAHIHI YA DAWA ZA KUFUBAZA VIRUSI VYA UKIMWI

 • Kuongezeka kwa kiasi kikubwa cha wingi wa virusi vinavyoshambulia mwili wa mgonjwa  wa UKIMWI,  Kutokuzingatia dawa hizi kwa kuruka dozi au kuacha kuzitumia kunaweza kupelekea kuongezeka kwa wingi wa virusi hivi kwa sababu dawa hizi hulenga kuzuia kuzaliana kwa vijidudu hivi

 • Kushusha kinga ya mwili (CD4), virusi vya ukimwi hulenga kushambulia na kuua chembechembe nyeupe za damu ziitwazo CD4 ambazo ni kinga ya mwili, hivyo basi kuzingatia dawa za kufubaza vijidudu hivi itapelekea kupunguza kushambuliwa kwa chembechembe hizi za damu na hivyo kukahikisha zinakuwepo kwa wingi ili kuimarisha kinga ya mwili.

 • Kuongeza hatari ya kushambuliwa na magonjwa nyemelezi, kinga ya mwili inaposhuka kwasababu ya kushambuliwa na vijidudu vya virusi vya ukimwi na kufikia CD4 200 au chini ya hapo mgonjwa anakua katika hatari ya kupata magonjwa nyemelezi,mwili nao unashindwa kukabiliana na magonjwa nyemelezi kama vile kifua kikuu,magonjwa ya kuhara.
 • Kuongeza kasi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa wengine- Kutokuzingatia matumizi ya daawa hizi huongeza Wingi wa virusi na kumuweka mgonjwa katika hatari kubwa ya kusambaza kwa watu wengine kupitia njia mbalimbali ikiwemo:ngono isiyo salama,kuchangia vitu vyenye ncha kali nk.

 • Kuongeza hatari ya kupata usugu wa madawa-kutokuzingatia matumizi sahihi ya dawa kwamfano kuacha dawa au kuruka dawa na baadae kuzirudia tena inasababisha kubadilika kwa maumbile ya vijidudu hivi na hivyo dawa kutokufanya kazi kama ilivyokusudiwa.

 • Kupunguza muda wa kuishi- Kwasababu vijidudu hivi huharibu kinga ya mwili na kufanya mwili kushindwa kukabiliana na magonjwa nyemelezi mgonjwa huugua mara kwa mara na baadae kufariki.

 

SABABU ZINAZOFANYA WATU KUTOKUZINGATIA MATUMIZI SAHIHI YA DAWA

 • Kuchoka kutumia dawa, kwasababu ni dawa za maisha na za mda mrefu, mgonjwa anashauriwa kutumia dawa hizi kila siku na kwa maisha yake yote,hivyo hupelekea mgonjwa kuzichoka na kukatisha dozi.

 • Kuogopa kuonwa kua ni muathirika wa virusi vya ukimwi kwa kuogopa kutengwa pale mgonjwa anapohudhuria clinic au kuchukua dawa.

 • Kukosekana kwa huduma za CTC kwa baadhi ya maeneo, dawa za kufubaza virusi vya ukimwi hutolewa katika vituo maalumu vya afya(CTC) na si vinginevyo. Hivyo hupelekea baadhi ya wagonjwa kushindwa kufika katika vituo hivyo kwasababu ya umbali.

 • Kukosekana kwa  mtu wa kuhimiza kutumia dawa hii ni kawaida kwa wagonjwa wengi kutokuzipenda dawa, hivyo inahitajika awepo mtu wa kutoa usaidizi kwa mgonjwa. Msaidizi huyu anapokosekana mgonjwa anaweza akasahau kutumia dawa kwa wakati sahihi.

 • Kutokua na elimu/uelewa juu ya madhara ya kutokuzingatia matumizi sahihi ya dawa hizi. Baadhi ya waathirika wa virusi vya ukimwi hawazingatii elimu waliyopewa kuhusu matumizi sahihi ya dawa hivyo hupelekea wagonjwa wengi kutokufuata masharti sahihi ya dawa kama walivyoshauriwa na wataalamu wa afya

 • Kutokuvumilia madhara yanayotokana na dawa hizo mfano kichefuchefu,kuhara,kukosa usingizi nk.

 • Msongo wa mawazo na magonjwa mengine ya akili, haya ni baadhi ya magonjwa yanayoweza kuathiri uwezo wa mgonjwa kuamua kufanya maamuzi sahihi na hivyo kushindwa kuzingatia matumizi sahihi ya dawa endapo mgonjwa atakosa usaidizi.

NAMNA YA KUONGEZA UZINGATIAJI WA MATUMIZI SAHIHI YA DAWA ZA KUFUBAZA VIRUSI VYA UKIMWI

 • Kutoa elimu ili kuelimisha jamii juu ya madhara yatokanayo na kutokuzingatia matumzi sahihi ya dawa
 • Kuweka mazingira rahisi na wezeshi ya upatikanaji wa dawa za kufubaza virusi vya ukimwi-uwezekano wa kuweka dawa katika maduka ya dawa(famasi) kwenye mazingira ambayo vituo maalumu vya afya (CTC) havipo au viko mbali.
 • Kuwajumuisha wanafamilia au msaidizi ambaye atakua tayari kumuhimiza mgonjwa  kuzingatia matumizi sahihi ya dawa
 • Kukubali hali ya ugonjwa na utayari wa kutumia dawa za Maisha
 • Kujenga uhusiano wa uaminifu kati ya mgonjwa na mtoa huduma za afya
 • Utengenezwaji wa dawa moja yenye mchanganyiko wa dawa zote ili kupunguza mzigo wa dawa

Leave a comment