Wafahamu mambo muhimu kuhusu Selimundu (Sickle cell)?

Wafahamu mambo muhimu kuhusu Selimundu (Sickle cell)?

Yapo magonjwa mengi ya  kurithi katika jamii na moja wapo ya magonjwa hayo ni ugonjwa wa seli mundu unaosababishwa na hitilafu katika seli nyekundu za damu.

Yafuatayo ni maelezo mafupi kuhusu ugonjwa huu hatari.

  • Ugonjwa wa seli mundu ni ugonjwa wa damu wa kurithishwa ,ambao husababisha seli nyekundu za damu kuwa ngumu na kuchukua umbo la mundu au mwezi mchanga.
  • Kwa kawaida seli nyekundu za damu huwa ni laini na za duara. Seli hizi za damu zina molekyuli ndani yake ziitwazo Himoglobini. Himoglobini huzisaidia seli nyekundu za damu kubeba hewa ya oksijeni kutoka kwenye mapafu na kuisafirisha kwenda sehemu mbalimbali za mwili.
  • Seli nyekundu za damu hubeba himoglobini aina ya HbA lakini zile za wagonjwa wa seli mundu hubeba Himoglobini aina ya HbS na hiki ndicho kiini cha Ugonjwa huu, na hitilafu ya kigenetiki wanayorithi wagonjwa hawa.

Uwepo wa himoglobini S (HbS) katika seli nyekundu za damu hupelekea seli hizo kuchukua umbo la mwezi mchanga(mundu). Kwa sababu ya umbo hili seli nyekundu za damu hupita kwa shida na kukwama katika mishipa midogo ya damu. Hali hii husabisha mgonjwa wa seli mundu kupata maumivu makali katika sehemu mbalimbali za mwili.

Pia seli nyekundu huishi mwilini kwa takriban siku mia moja na ishirini wakati zile za mgonjwa wa seli mundu huishi kwa siku kumi na sita tu. Hii huchangia kupungua kwa seli hizo na kupata upungufu wa damu mara kwa mara.

Bahati nzuri dalili za ugonwja huu hazijionyeshi kwa mtoto mchanga kwani watoto wadogo wana aina nyingine ya himiglobini inayowakinga dhidi ya dalili hizo.

Ugonjwa wa seli mundu ni ugonjwa hatari unaihitaji msaada wa kipekee. Wazazi, walezi na pia mgonjwa mwenyewe wanapaswa kuwa na elimu ya ugonjwa huu ili kufahamu namna bora ya kuishi. Ni muhimu kuepuka kuwanyanyapaa wagonjwa hawa.


Leave a comment